1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatangaza kuanza kusafisha sajili ya wakimbizi

12 Juni 2023

Serikali ya kenya imetangaza kuanza kusafisha sajili ya wakimbizi katika kambi za wakimbizi za Kakuma na Daadab kuafuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya Wakenya waliojisajili kama wakimbizi.

Kakuma, Kenya | Media Development
Picha: Laura Wagenknecht

Wengi wa wakenya katika maeneo hayo, walishawishika kujisajili kama wakimbizi ili kunufaika na vyakula na vifaa vingine vilivyokuwa vikitolewa na shirika la umoja wa kimatifa la kuwashugulikia wakimbizi UNHCR. Kwa sasa, wengi wao wameshindwa kupata vitambulisho vya kitaifa.

Wakenya wajisajili kama wakimbizi kunufaika na misaada

Tangu ujio wa kambi za wakimbizi nchini Kenya miaka ya tisini, idadi kubwa ya Wakenya kutoka Jamii zinazowapa wakimbizi hao hifadhi, imekuwa ikijisajili kama wakimbizi ili kufaidika na huduma zinazotolewa kwa wakimbizi na mashirika ya kiutu.

vijana wengi wakosa vitambulisho

Ila hatua yao ya kujisajili kama wakimbizi, imeendelea kuwanyima wengi wa vijana fursa ya kupata huduma za serikali ikiwemo kupata vitambulisho vya kitaifa.

Baadhi ya vijana wajutia kujiandikisha kama wakimbizi

Baadhi ya vijana wanakiri kuwa,walishawishika kujisajili kama wakimbizi kwa ajili ya maslahi ila wengi wao kwa sasa wanaishi kwa majuto.

Wakimbizi waliotoroka Sudan katika kituo cha Renk, Sudan KusiniPicha: JOK SOLOMUN/REUTERS

Serikali yaendeleza shughuli za kuwaunganisha wakimbizi

Serikali ya Kenya imekuwa ikiendeleza shughuli za kuwaunganisha wakimbizi na Jamii zinazowahifadhi kama sehemu ya kukomesha uhasama ambao umekuwa ukiripotiwa kila wakati baina yao.

Vijana wengi katika kambi waiomba serikali msamaha

Vijana wengi kutoka Daadab na Kakuma kwa wakati huu wanairai serikali kuwasamehe na kuondoa majina yao katika sajili ya wakimbizi ili waendeleze Maisha yao kama wakenya wengine. Carlos Eipa ni mwathiriwa raia wa Turkana kutoka Kakuma.

Serikali pia inabaini kuwa angalau Wakenya elfu kumi na watano kutoka maeneo ya Kakuma na Daadab walijisajili kama wakimbizi.

Majina ya Wakenya kwenye sajili kuondolewa

Kulingana na kamishna mkuu anayesimamia masuala ya wakimbizi hapa nchini John Burugu, zoezi la kusafisha sajili ya wakimbizi inaendelea na kwamba hivi karibuni,majina ya Wakenya yaliyoko kwenye sajili hiyo yataondolewa. Kwa sasa, Wakenya waliosajiliwa kama wakimbizi wataendelea kukosa huduma hizo hadi serikali itakapokamilisha zoezi la kusafisha daftari lake rasmi la wakimbizi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW