1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seikali ya Kenya kwanza kukabiliana na vitisho Kenya

17 Agosti 2022

Serikali ya Kenya Kwanza imeahidi kuongoza pasina vitisho na kudumisha demokrasia. Wakati huohuo, naibu wa rais mteule Rigathi Gachagua ameweka bayana kuwa wako tayari kwa kitakachotokea mahakamani.

Wahlen in Kenia I William Ruto
Picha: Thomas Mukoya /REUTERS

Ifahamike kuwa Azimio la Umoja One Kenya inapinga matokeo ya uchaguzi uliowanyima ushindi na wanaelekea kwenye mahakama ya juu. Akiwa kwenye makaazi yake rasmi ya Karen, rais mteule William Ruto aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali yake haitamuonea yeyote na kuwa vitisho vitakoma katika kipindi hiki.

Rais mteule wa Kenya alikutana na viongozi walioibuka washindi kwenye uchaguzi mkuu uliopita. William Ruto aliwasihi viongozi hao kuja pamoja kwa manufaa ya taifa.Ruto alisisitiza kuwa mikakati inaandaliwa kuwawajibisha mawaziri mbele ya bunge kinyume na ilivyo sasa.

Kambi ya Kenya kwanza iko tayari kwa uamuzi wa mahakama.

Mgombea aliyeshindwa Raila OdingaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Wakati huo huo, naibu wa rais mteule Rigathi Gachagua ameweka bayana kuwa wako tayari kwa chochote kitakachotokea mahakamani. Kauli hizo zinatolewa wakati ambapo Azimio la Umoja One Kenya inajiandaa kuelekea kwenye mahakama ya juu kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliowanyima ushindi.

Alasiri hii, mgombea wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya alikutana na viongozi wa kambi yake walioibuka washindi kwenye jumba la mikutano la KICC. Mgombea mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya Martha Karua alisisitiza kuwa ushindi ni wao ila umecheleweshwa tu.

Kwenye kikao hicho ambacho kilidhamiria viongozi kufahamiana, waziri kiongozi mtarajiwa Kalonzo Musyoka alishikilia kuwa azma yao iko pale pale.

Siku saba za mbivu na mbichi za Raila Odinga.

Azimio la Umoja One Kenya ina siku saba tangu mshindi wa uchaguzi wa urais alipotangazwa Agosti 15 kuwasilisha kesi kwenye mahakama ya juu.

Yote hayo yakiendelea,wajumbe wa mataifa ya kigeni walioko Kenya wanawatolea wito wanaodai kuibiwa ushindi kwenye uchaguzi mkuu uliopita kufuata mikondo ya haki.Kwenye taarifa yao ya pamoja,wajumbe hao wamewarai wanasiasa kudumisha amani.Wajumbe hao wanawakilisha mataifa ya Ulaya ikiwemo Ujerumani.

Soma zaidi:Odinga akataa kuutambua ushindi wa William Ruto

Kwa upande mwengine,wabunge 10 huru na wanaojitegemea wanaripotiwa kujiunga na muungano wa rais mteule wa Kenya Kwanza.Ifahamike kuwa Kenya Kwanza ina wingi wa viti kwenye baraza la Senate ila kwenye bunge la taifa Azimio ndio iliyo mstari wa mbele.TM,DW Nairobi.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi