1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kenya yaanza mchakato wa kufidia jamii ya Ogiek

19 Januari 2023

Baada ya miaka mingi ya kusaka haki, serikali ya Kenya imeanza mchakato wa kuifidia jamii asilia na ya wachache ya Ogiek baada ya uamuzi wa mahakama ulioipata na hatia ya ukiukaji wa haki zao.

Kenia Wahlkampf Kenya Kwanza Alliance William Ruto Rigathi Gachagua
Picha: Press service William Ruto

Baada ya miaka mingi ya kutafuta haki, kutokana na hatua ya serikali ya Kenya kuwafurusha kutoka msitu wa Mau wanaosema ni ardhi ya mababu zao, Jamii asilia ya Ogiek ilipata ahueni pale mahakama ya bara la Afrika ya kushughulikia haki za binadamu, ilioko nchini Tanzania, ilipoamua kwamba serikali ya Kenya ilikuwa imekiuka haki zao za kibinadamu. Uamuzi huo wa mwezi Juni mwaka 2022, uliorodhesha namna serikali itatekeleza fidia yenyewe ikiwemo kuwarejesha Ogiek msituni Mau na kuwalipa fidia shilingi milioni 150, ila serikali imekuwa ikisuasua .

Tume ya utekelezaji haki yaandaa mkutano wa utekelezaji wa uamuzi wa mahakama 

Ila sasa Tume ya utekelezaji haki nchini imeandaa mkutano wa mashauriano ulioshirikisha wizara nne na afisi ya mwanasheria mkuu kuratibu mikakati ya kutekeleza uamuzi wa mahakama hiyo. Mercy Wambua afisa mkuu katika tume hiyo anaeleza kwamba wako tayari kuratibu mikakati ili kuhakikisha jamii hiyo ya wachache inapata haki. Bi Wambua amesema kwamba wako tayari  kuwasaidia Wakenya, na jamii zilizotengwa, kuweza kufikia afisi za umma na kwamba watawapa mwongozo na ufafanuzi wa michakato ya utekelezaji na magumu yoyote wanayokumbana nayo wanapozuru kwenye afisi hizo.

Utekelezwaji wa uamuzi ulicheleweshwa na kipindi cha uchaguzi

Uamuzi huo ulitarajiwa kutekelezwa katika muda wa miezi sita na serikali kuwasilisha ripoti katika mahakama hiyo kuhusu hatua ilizopiga katika utekelezaji wa uamuzi huo. Afisi ya Mwanasheria mkuu wa Kenya, imeeleza kwamba kuchelewa kutekelezwa kwa uamuzi huo, kulitokana na msimu wa uchaguzi na shughuli ya serikali ya mpito. Christopher Marwa, mwakilishi wa afisi ya mkuu wa sheria amesema kile anachoweza kusema ni kwamba sasa kuna katibu mkuu mpya kwenye nafasi hiyo, na watahitaji muda wa kuuchambua uamuzi wa mahakama, na kisha kutoa msimamo wao wa namna maagizo ya mahakama yatakavyotekelezwa.

Mahakama yaagiza serikali kushauriana na jamii ya Ogiek

Mahakama hiyo vile vile iliagiza serikali kuitambua na kushauriana na jamii hiyo ya Ogiek kuambatana na tamaduni na kanuni zao kuhusu masuala ya mazingira, maendeleo na uwekezaji katika ardhi yao. Daniel Kobei, mwenyekiti wa shirika linalotetea haki na maendeleo ya jamii ya Ogiek linalofahamika kama OPDP, anasema muhimu sana kwa jamii hiyo ni kwamba watambulike. Anasema jamii ya Ogiek ina uwezo wa kuchangia pakubwa uhifadhi wa msitu wa mau kupitia desturi na tamaduni zao.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW