1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idara ya huduma za feri yalaumiwa kwa mkasa wa Feri

4 Oktoba 2019

Wabunge nchini Kenya wanaishinikiza serikali kuu kuchukua hatua baada ya mkasa wa kuzama kwa gari katika kivuko cha Likoni kusababisha maafa mwanzoni mwa wiki hii

Kenia Mombasa Fähre
Picha: DW/E. Ponda

Kamati ya bunge ya uchukuzi inashinikiza viongozi wa huduma za pantoni nchini Kenya, KFS kujiuzulu kufuatia ajali ya siku chache zilizopita kwenye kivuko cha Likoni.

Akiwa kikaoni hapo jana, mratibu wa wizara ya uchukuzi Chris Obure alikiri mbele ya kamati ya bunge ya uchukuzi kuwa ajali hiyo ingeepukika kama tahadhari zingechukuliwa.

Hata hivyo alisisitiza kuwa juhudi sasa bora zijikite kwenye uopoaji wa maiti badala ya kulaumiana. Ifahamike kuwa kikosi cha wanamaji cha Kenya Navy kina makao yake eneo la Mtongwe lililo karibu na Likoni walikokufa maji mama na mwanawe mwanzoni mwa wiki hii.

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alimrai Rais Uhuru Kenyatta kuahirisha sherehe za Mashujaa zilizopangwa kufanyika baadaye mwezi huu ili kuomboleza na Wakenya.

Idara ya huduma za feri yalaumiwa

Baadhi ya wakenya wakiwa katika kivuko cha feriPicha: DW/E. Ponda

Wabunge hao waliituhumu idara ya huduma za feri, KFS kwa uzembe, utepetevu na kutowajibika ukizingatia hatua ziilizochukuliwa tangu mkasa kutokea siku 4 zilizopita. Kwa upande wake mbunge wa Likoni ilikotokea ajali Mishi Mboko anaishauri idara ya KFS kuwasilisha ombi la kutengewa fedha za ziada kutoka kwa serikali kuu.

Mbunge wa Lamu Magharibi Kapteni Ruweida Obbo alisikitishwa na kasi ya operesheni ya kuopoa maiti na kuweka bayana kuwa upo umuhimu wa kuwatumia walio na ujuzi na kutolea mfano vijana wa Kizingiti wa kaunti ya Lamu.

Mwenzake wa Lungalunga Khatib Mwashetani anasisitiza kuwa feri zinazotumika ni mbovu na mpya zinahitajika.

Kivuko cha Likoni kina kina kirefu na ni eneo la pitepite nyingi. Juhudi za kuopoa maiti zinatatizwa na mvua inayoendelea kunyesha. Zaidi ya watu laki tatu na magari alfu 6 hutumia kivuko cha Likoni kuingia na kutoka kisiwani Mombasa kila siku.

Chanzo: Thelma Mwadzaya

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW