1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kenya yatakiwa kupeleka fedha majimboni haraka

Shisia Wasilwa
25 Aprili 2023

Baraza la Magavana Kenya limeipa serikali siku 14 kutoa shilingi bilioni 94 kwenye serikali za majimbo 47 la sivyo watasitisha huduma kwenye majimbo hayo kutokana na kuchelewa kwa serikali kuwapa fedha za miezi mitatu.

Kenia Präsident William Ruto
Picha: TONY KARUMBA/AFP

Magavana hao wameitaka Wizara ya Fedha kuwalipa fedha za miezi Februari, Machi na Aprili ili watoe huduma kwa wananchi. Taarifa ya Baraza la Magavana inajiri wakati wafanyikazi wa kaunti pamoja na watumishi wa umma kucheleweshewa mishahara yao, hali inayotishia utendakazi kwenye majimbo na mashirika ya serikali nchini Kenya.

Kwenye taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, magavana hao wanaitisha malimbikizi ya shilingi bilioni 31 za mwezi Februari, shilingi bilioni 29 za mwezi Machi na shilingi bilioni 47 za mwezi Aprili.

Magavana wadai serikali inahatarisha mfumo wa ugatuzi

Jamii ya wafugaji katika jimbo la MarsabitPicha: Michael Kwena/DW

Sasa magavana hao wanasema hatua ya serikali inahatarisha mfumo wa uongozi wa ugatuzi. Ann Waiguru ambae ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana amesema "Tunawafahamisha wananchi wa Kenya, kuwa kutokana na kuchelewa kutolewa kwa fedha na serikali Kuu, Serikali za majimbo hazitafanya kazi kama inavyostahili.”

Tangu mfumo wa ugatuzi uanze kutekelezwa nchini Kenya mwaka 2010, mishahara ya wafanyikazi wa majimbo haijawahi kuchelewa kwa miezi mitatu. Aidha tangu taifa lijinyakulie uhuru mwaka 1963, mshahara wa wafanyakazi wa umma haujawahi kuchelewa, ishara kuwa serikali ya sasa inakabiliwa na changamoto za kifedha.

Serikali ya Kenya yatakiwa kutoa fedha haraka

Magavana hao wanaitaka Wizara ya Fedha kutoa fedha hizo haraka iwezekanavyo. Muthomi Njuki ni mwenyekiti wa kamati ya Afya kwenye Baraza hilo la Magavana amesema "Tunatoa tahadhari kwa serikali kuu na kuwafahamisha Wakenya, kwamba hatuna chaguo lakini kusitisha operesheni kwenye majimbo, hadi majimbo yafadhiliwe.”

Kwenye mkutano huo wa kila mwaka magavana hao pia walichukua nafasi hiyo kuwasuta maseneta ambao walikataa kuunga mkono mswada wa Ugavi wa mapato wa mwaka 2023. Iwapo mswada huo ungepitishwa kiasi cha fedha ambazo serikali kuu hutengea majimbo kingeongezeka kutoka shilingi bilioni 370 hadi shilingi bilioni 407.

Soma zaidi:Waliokufa kwa njaa Kenya wafikia watu 73

Waiguru anafafanua alifafanua kwa kusema kwamba "Tuna wasiwasi mkubwa kwa sababu katika historia ya ugatuzi, bunge la Seneti halijawahi kupiga kura kinyume na moyo wa kuimarisha ugatuzi haswa kuongezwa kwa raslimali.”

Magavana hao wamehimiza bunge la Seneti kudumisha majukumu yao ya msingi na kuhakikisha kuwa majimbo yanapata mgao wao ili kuimarisha utendakazi. Serikali ya Rais William Ruto imejitetea kuwa haikupata fedha za kutosha kwenye hazina kuu ilipochukua usukani, huku ikishikilia kuwa haitakopa fedha ili kulipa mishahara. Wauguzi na madaktari wametishia kugoma kutokana na ukosefu wa mishahara.

DW Nairobi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW