1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kenya yawatafuta watu 50 waliotoroka karantini

22 Aprili 2020

Serikali ya Kenya inawatafuta watu 50 wanaoaminika kutoroka eneo walikowekwa karantini jijini Nairobi. Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali inawafahamu watu hao na kwamba, watakapopatikana watarejeshwa karantini.

Kenia Coronavirus Uhuru Kenyatta
Picha: PSCU

Rais Kenyatta ameyasema hayo alipokuwa akihojiwa na vyombo vya habari nchini Kenya, leo asubuhi ambapo aliwaonya watu wenye nia ya kutoroka kwenye karantini. Aidha alisema kuwa nia ya kuzingatia karantini ni kupunguza kusambaa kwa ugonjwa wa Covid 19. Watu hao 50, wanasemekana kutoroka kwenye chuo cha mafunzo ya matibabu cha Nairobi, usiku, wakati mvua kubwa zilipokuwa zikinyesha. 

Duru zinasema kuwa watu walisikika wakilalamika kuhusu fedha nyingi walizotarajiwa kutozwa kwa siku 14 ambazo wangezuiliwa kwenye kituo hicho. Kituo hicho kinatoza dola 20 sawa na shilingi elfu mbili kwa siku. Hayo yanajiri wakati watu wengine 32 kuripotiwa kutoroka katika karantini iliyoko katika jimbo la Mandera, katika mazingira ya kutatanisha. Daktari Mercy Mwangangi ni Katibu wa kudumu katika wizara ya Afya.

“Yeyote atakayevunja sheria za kuwataka watu wabakie majumbani, atachukuliwa kuwa amekutana na mtu mwenye virusi vya corona, hivyo atawekwa kwenye karantini kwa kipindi cha siku 14;” alisema Daktari Mercy Mwangangi.

Watu wanaopatikana nje baada ya saa moja za usiku, polisi huwakamata na kuwaweka kwenye karantini, huku wakigharamia muda wao kule ndani.

Baadhi ya Wakenya wanalalmikia hatua ya serikali ya kudhibiti virusi vya Corona

Baadhi ya Wakenya wakipita katika eneo linalowanyunyizia dawa ya kuuwa vijidudu nchini humoPicha: DW/F. Musa Abdalla

Huku wizara ya Afya, ikichukua hatua hiyo kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo, baadhi ya wakenya wanahisi kuwa polisi wanakula njama na baadhi ya vituo hivyo ili kuwatoza hela pamoja na kuwanyanyasa. Idadi kubwa ya vijana wamekuwa wakikamatwa kwa kutozingatia amri ya kutotoka nje ifikapo saa moja za usiku. Baadhi ya watu walioko kwenye karantini wamedai kuwa mazingira mle sio mazuri.

"Maana ukikamatwa na Corona utaiambia nini heri utashikwa na polisi utakuwa na la kumwambia, eti nimekwenda dukani nimechelewa kazini, nnavyoangalia ni kwamba ni kama yale mazoea ya punda na mkia wake wakenya hawaelewi ile hatari inayowakodolea macho kwahiyo nawasihi ndugu zangu wafuate taratibu za serikali;" alisema Felix Oduor mtaalamu wa masuala ya matibabu nchini Kenya.

Idadi ya visa vya watu wenye virusi vya Corona kote nchini imefikia 296 baada ya watu wengine 15 kugunduliwa Jumanne. Idadi hiyo iliongezeka baada ya watu 545 kuchunguzwa. Kufikia Jumanne watu 14,417 walikuwa wamepimwa kote nchini. 

Wakenya waliokwama Uingereza wanaweza kurejea  nyumbani kwa gharama zao binafsi

Wakati huo huo, Wakenya waliokwama Uingereza na wangependa kurejea nchini kwa nauli zao, wana nafasi ya kufanya hivyo siku ya Jumamosi. Shirika la Ndege la Kenya litakuwa likiwasafirisha. Uamuzi huo uliafikiwa baada ya mazungumzo kati ya serikali ya Kenya na balozi wa Kenya nchini Uingereza.

Raia wa Kenya pekee ndio watakaoruhusiwa kuabiri ndege hiyo, ikirejea katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Shirika hilo la ndege limesema kuwa abiria wote watapimwa iwapo wana virusi vya Corona, pindi tu watakapopokea tiketi za usafiri. 

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW