1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Lebanon yajiuzulu kufuatia mripuko wa Beirut

11 Agosti 2020

Waziri Mkuu wa Lebanon Hassan Diab ametangaza kujiuzulu kwa serikali yake jana jioni, akisema mripuko mkubwa ulioutikisa mji wa Beirut hivi karibuni, na kusababisha hasira ya umma ulitokana na ufisadi mkubwa.

Libanon Proteste in Beirut
Picha: Reuters/G. Tomasevic

"Leo tunafuata matakwa ya watu wa Lebanon, ya kuwawajibisha wale waliohusika na maafa haya,” alisema waziri mkuu Hassan Diab katika hotuba yake wakati akitangaza kujiuzulu kwa serikali yake. Ameongeza kuwa maafa hayo yametokana na mfumo wa ufisadi, huku akisema kuwa wale waliohusika wanapaswa kuona aibu kwasababu, matendo yao yamesababisha janga kubwa lisiloweza kuelezeka.

Tayari rais Michel Aoun ameikubali barua ya kujiuzulu ya serikali ya Diab iliyoundwa mwezi Januari na kuungwa mkono na kundi kubwa lililo na nguvu nchini humo linaloungwa mkono na Iran la hezbolla na washirika wake, lakini ameiomba ibakie kuwa serikali ya muda au ya mpito hadi pale baraza jipya la mawaziri litakapoteuliwa.

Kulingana na mfumo wa serikali, rais Aoun anatarajiwa kuwasiliana na wabunge kujua ni nani atakaekuwa waziri mkuu mpya na kisha kumpa nafasi hiyo mgombea atakaekuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wabunge.

Mgogoro wa kisiasa na kiuchumi huenda ukaufanya mchakato wa kumtafuta Waziri Mkuu kuwa mgumu zaidi

Waziri Mkuu wa Lebanon Hassan DiabPicha: Reuters/M. Azakir

Kuunda serikali wakati kukiwa na mivutano na migawanyiko imekuwa changamoto kubwa hapo awali, lakini kwa sasa kutokana na kuongezeka kwa mashaka na kutouamini utawala uliopo hasa kutokana na mripuko wa hivi karibuni na kukuwa kwa mgogoro wa kisiasa huenda ikawa vigumu kumpata mgombea atakaetaka kuwa waziri mkuu.

Wakati hatua ya Diab ikinuiwa kujibu hasira za watu kuhusu mripuko wa Beirut inaonekana pia kuitumbukiza zaidi Lebanon katika mgogoro wa kisiasa na inaweza kuathiri zaidi mazungumzo yaliosimama kati ya taifa hilo na shirika la kimataifa la fedha duniani IMF kuhusiana na mipango ya kuuokoa uchumi wa taifa hilo.

Mazungumzo hayo yalioanza mwezi Mei yalisitishwa kutokana na serikali kushindwa kutekeleza mabadiliko yaliohitajika na mvutano uliokuwepo kati ya serikali hiyo na mabenki na wanasiasa juu ya kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo.

Mripuko uliotokea Agosti nne katika bandari ya Beirut, uliosababishwa na kile serikali inachosema ni tani 2000 za kemikali ya ammonium nitrate, uliwauwa watu 163, kuwajeruhi watu zaidi ya 6000 na kuuharibu kabisa mji wa nchi hiyo inayokumbwa na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi.

Chanzo: Amina Abubakar/afp/reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW