1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Lebanon yakubali kuwaondoa Hizbullah kusini

30 Septemba 2024

Serikali ya Lebanon imesema ipo tayari kulitekeleza kwa ukamilifu azimio la Umoja wa Mataifa lenye lengo la kuondolewa kwa Hizbullah kusini mwa Mto Litani kama sehemu ya makubaliano ya kusimamisha mapigano na Israel.

Lebanon Najib Mikati
Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati.Picha: Mohamed Azakir/REUTERS

"Sisi, Lebanon, tupo tayari kulitekeleza Azimio Namba 1701 na mara tu baada ya mapigano kusimamishwa tutakuwa tayari kulipeleka jeshi la Lebanon kusini mwa Mto Litani kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa kushirikiana na jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Mataifa," alisema Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati.

Wakati huo huo, wapiganaji wa Hizbullah wamesema wako tayari kukabiliana na uvamizi wowote wa ardhini wa Israel dhidi ya Lebanon.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

01:03

This browser does not support the video element.

Naibu kiongozi wa kundi hilo, Naim Qassem, ameyasema hayo katika hotuba yake ya kwanza hadharani tangu Israel ilipomuua kiongozi wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, wiki iliyopita.

Qassem alizungumza kutokea eneo lisilojulikana wakati Israel ikiendelea na mashambulizi ya anga kwenye mji wa Beirut na kwingineko nchini Lebanon.

Nini kinafuata Lebanon baada ya mauaji ya Nasrallah?

This browser does not support the audio element.

Makamanda kadhaa wa Hizbullah wameuliwa kutokana na mashambulizi ya Israel katika wiki mbili zilizopita.

Israel imewauwa pia zaidi ya watu wengine 1,000, wakiwemo wanawake na watoto, kwenye mashambulizi hayo yaliyosababisha wengine zaidi ya milioni moja kuyakimbia makaazi yao.