1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Lebanon yatoa wito wa usitishwaji mapigano

11 Oktoba 2024

Serikali ya Lebanon imetoa wito siku ya Ijumaa wa kutaka kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah. Hii ni baada ya makumi ya watu kuuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika shambulio mjini Beirut.

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib MikatiPicha: Mohamed Azakir/REUTERS

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameutolea wito hivi leo Umoja wa Mataifa kupitisha azimio linalotaka usitishwaji mapigano mara moja kati ya Israel na Hezbollah, na kwamba ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuwasilisha ombi hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Waziri Mkuu huyo wa Lebanon amelaani pia mashambulizi ya Israel kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa katika mji wa Naqoura kusini mwa Lebanon.

"Shambulio dhidi ya vikosi vya UNIFIL ni uhalifu ambao tunaulaani na ni jukumu la jumuiya ya kimataifa, ambayo hadhi yake imekiukwa na uwepo wake unatishiwa kutokana na kulengwa kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa."

Soma pia: Israel yakosolewa kwa kushambulia kituo cha UNIFIL

Aidha, Mikati amesema mambo yanayoendelea hayakubaliki na kwamba Lebanon ni muhanga wa kiburi cha Israel ambayo inakiuka uhuru wa taifa lake huku ulimwengu ukishuhudia katika ukimya unaotia mashaka kuhusu mauaji ya Israel.

Rais wa Iran Massoud PezeshkianPicha: Dolat.ir

Katika muendelezo wa kauli kama hizo, Rais wa Iran Massoud Pezeshkian amesema Israel inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi, inatakiwa kusitisha mauaji ya watu wasio na hatia. Shambulio la jana usiku la Israel katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut liliwaua watu 22 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 100.

Hata hivyo,  Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati  ameongeza kusema kuwa suluhisho la kidiplomasia liko mezani, na Hezbollah ambayo ni mshirika katika serikali ya Lebanon imeafiki kuendelea kuliunga mkono azimio nambari 1701 ya Umoja wa Mataifa ambalo linapiga marufuku uwepo wa wanamgambo wa Hezbullah katika eneo linalopakana na Israel.

Azimio hilo linatoa mamlaka pekee kwa jeshi la Lebanon na Vikosi vya Muda vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL kusimamia usalama eneo hilo, jambo ambalo linawataka wanajeshi wa Israel kuondoka ndani ya ardhi ya Lebanon.

Viongozi wa nchi za Bahari ya Mediterania wakutana

Mapigano yaendelea katika Ukanda wa Gaza na nchini Lebanon.Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Wakati mapigano yakiendelea katika Ukanda wa Gaza na nchini Lebanon, viongozi kutoka nchi tisa za Ulaya zilizopo karibu na Bahari ya Mediterania wamekutana hivi leo nchini Cyprus kujadili vita vya  Mashariki ya Kati , ambavyo wanahofia vitachochea uhamiaji na kutishia usalama wa mataifa hayo. Wakuu wa nchi au serikali kutoka Ufaransa, Italia, Uhispania, Ureno, Ugiriki, Cyprus, Malta, Slovenia na Croatia walijumuika na Mfalme wa Jordan Abdullah II, kwa mkutano huo wa siku moja katika mji wa Cyprus wa Paphos.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anatarajiwa mwishoni mwa wiki ijayo kusafiri hadi nchini Uturuki ambako anatarajiwa kukutana na Rais Tayyip Erdogan ili kujadili miongoni mwa mambo mengine, vita vya Mashariki ya Kati na masuala ya uhamiaji.

(Vyanzo: DPAE, AP, AFP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW