Serikali ya Libya imeahidi kuitisha uchaguzi
20 Aprili 2011Mapema asubuhi sauti ya Obeid ilisikika kupitia shirika la utangazaji la Uingereza BBC ikisema"kama mashambulizi yatasimamishwa,kutafanyika uchaguzi baada ya miezi sita ambao utasimamiwa na Umoja wa Mataifa".
Waziri huyo wa Mambo ya Nje amesema uchaguzi utaziba nyufa zote,kila kitu kitakwenda mezani ikijumuisha hatima ya Ghadhafi kama kiongozi wa Libya.
Al Obeid amesisitiza kwamba Libya imelitilia maanani suala la kusitishwa mapigano ambalo linanisamiwa na waangalizi wa nje lakini pia amekosoa kitendo cha Uingereza kutuma maafisa wa kijeshi nchini humo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa waasi.
Jana Uingereza ilisema itapeleka maafisa kadhaa nchini Libya kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna ya kujipanga pamoja na mawasiliano lakini haitawapa silaha waasi wala kuwafunza kupigana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague anasema bado wanasimamia utekelezaji wa maadhimo ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
"Kila tunachokifanya kiko katika mipika ya azimio la Baraza la Usalama namba 1973.hazimio hilo linatupa mamlaka sisi na mataifa mengine kuchukua hatua zozote muhimu kuwalinda raia na umma nchini Libya."alisema Hague
Obeid ameita kitendo hicho kutoa mafunzo ni kuendeleza kudumisha mapigano.
Nae Kiongozi wa Waasi huko Benghazi Nuri Abdullah Abdullati ameziomba Uingereza na Ufaransa kutuma vikosi kwa ajili ya kukabiliana na wanajeshi watiifu kwa kanal Gadhafi ambao wameuzingira mji wa Misrata.
Taarifa kutoka huko Benghazi zinasema idadi ya watu walikufa nchini Libya kutokana na mapigano hayo katika kipindi cha miezi miwili zinafikia kiasi ya watu 10,000.
Mashambulizi yaneandelea nchini Libya, ndege za kivita za NATO zimeshambulia miundombinu ya mawasiliano na utangazaji katika miji kadhaa nchini humo.
Kituo cha televisheni cha serikali cha Al-Libiya hakikutoa ufafanuzi wa kina wakati mashambulizi hayo yakifanyika.
Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Tunisia imesema makombora ya manee ya mizinga kutoka nchini Libya yameshambulia eneo la meta 500 kutoka mpakani mwa Libya.Hata hivyo hakuna majeruhi aliyeripotiwa.
Nchi hiyo imekuwa ikipokea maelfu ya wakimbizi kwa siku, kutoka Libya,ambao wengi wao wanaingilia upande wa kusini kutokea mkoa wa Dehiba.
Kwa upande mwengine Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo anakutana na kiongozi wa Waasi,Mustafa Abdel Jalil mjini Paris kujadili masula kadhaa likiwemo la NATO kuongeza nguvu dhidi ya Ghadhafi.
Nayo mapigano kati ya wanajeshi watiifu kwa Gaddafi na Waasi yanaripotiwa kuendelea katika maeneo ya magharibi ya miji ya Ajdabiyah na mashariki mwa Libya.
Mwandishi:Sudi Mnette RTR/APE
Mhariri: Abdul-Rahman