1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Libya yapoteza udhibiti wa mji mkuu

Josephat Nyiro Charo1 Septemba 2014

Serikali ya mpito ya Libya inayoondoka madarakani imekiri leo (01.09.2014) kwamba imepoteza kabisa udhibiti wa mji mkuu, Tripoli kwa makundi ya waasi. bunge limemtaka waziri mkuu aunde serikali mpya.

Abdullah al-Thani Libyen Regierungschef 03.06.2014
Picha: AFP/Getty Images

Serikali hiyo inayoongozwa na Abdullah al-Thani, ambayo ilijiuzulu wiki iliyopita, imesema makundi ya waasi wenye silaha, wengi wao wakiwa wanamgambo wa kiislamu, wamezidhibiti wizara na wanawazuia wafanyakazi wa serikali. Katika taarifa yake iliyotoa ikiwa mafichoni mashariki mwa nchi hiyo, serikali hiyo imesema wizara na ofisi zake zimechukuliwa na makundi ya waasi ambao wanawazuia wafanyakazi wa serikali wasiingie na wanawatisha wakuu wao. Imesema serikali ya mpito imekuwa ikiwasiliana na maafisa wake na inajaribu kuhakikisha utoaji wa huduma unaendelea bila kutatizwa.

Libya imetumbukia kwenye machafuko tangu kuondolewa madarakani na kuuwawa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo hayati Muammar Ghadafi, miaka mitatu iliyopita, huku tawala za mpito zikikabiliana na makundi ya waasi yenye nguvu yaliyopigana kumng'oa kiongozi huyo. Libya imekuwa ikipoteza udhibiti wa maeneo kwa waasi na muungano wa wapiganaji wa kiislamu, Fajr Libya - Libya Dawn, uliouteka uwanja wa ndege wa Tripoli mnamo Agosti 22 baada ya wiki za mapigano makali na wapiganaji mahasimu wazalendo.

Ubalozi wa Marekani wavamiwa

Hapo jana wanamgambo waliingia katika uwanja wa ubalozi wa Marekani mjini Tripoli ambao wafanyakazi wake walihamishwa tangu mwishoni mwa mwezi Julai, huku vidio zikiwaonyesha wanaume wakiruka kutoka roshani na kupiga mbizi katika dimbwi la kuogelea. Wanachama wa muungano wa Fajr Libya wamesema walikwenda kulilinda eneo hilo kusini mwa Tripoli kuepusha uporaji.

Mapigano katika mji wa TripoliPicha: Reuters

Hassan Ali, kamanda wa kikosi kinachoulinda uwanja wa ubalozi wa Marekani, "Tulikuja hapa tukawakuta wapiganaji wa kundi la Zintan Brigades tuliokuwa tukiwafukuza. Kulitokea makabiliano kidogo ya risasi na kukatokea uharibifu mdogo. Tuliingia ndani na kuwaweka baadhi ya wapiganaji wetu kulikomboa eneo hili na tumejitahidi kulilinda kadri ya uwezo wetu."

Hata hivyo balozi wa Marekani Deborah Jones, ambaye sasa ametumwa nchini Malta, amesema katika mtandao wa kijamii wa Twitter hakukuwa na dalili zozote jengo la ubalozi wa Marekani mjini Tripoli lilikuwa limeharibiwa.

Waziri mkuu atakiwa kuunda serikali

Wakati haya yakiarifiwa shirika rasmi la habari la Libya, LANA, limeripoti kwamba bunge la nchi hiyo hii leo limemtaka waziri mkuu aliyejiuzulu hivi majuzi, Abdullah al Thinni kuunda serikali mpya. Kwa mujibu wa afisa wa serikali bunge limepiga kura katika mji wa mashariki mwa Tobruk kumtaka al Thinni aunde timu ya mawaziri 18 badala ya 30 wa serikali inayoondoka madarakani. Afisa huyo aidha amesema saba kati ya mawaziri wapya wataunda baraza la dharura la mawaziri litakaloshughulikia matatizo yanayoikabili Libya kwa sasa.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW