Serikali ya mpito Libya yajiuzulu
29 Agosti 2014Serikali ya Waziri Mkuu, Abdullah al-Thinni, imesema bunge lililochaguliwa hivi karibuni litachukua jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri. Katika taarifa yake, serikali hiyo imesema imewasilisha barua ya kujiuzulu kwa bunge na lina imani kuwa bunge jipya litaichagua serikali mpya itakayojumuisha makundi yote ya wananchi wa libya.
Hatua hiyo imetokea siku chache baada ya Bunge la Taifa ambalo muda wake ulimalizika mwezi Februari mwaka huu, kukutana mjini Tripoli, mkutano ulioitishwa na wanamgambo wa Kiislamu. Bunge hilo limemteua Profesa Omar al-Hassi ambaye ni profesa wa chuo kikuu, kuwa waziri mkuu wa serikali ya uokozi wa taifa.
Baraza la wawakilishi lililochaguliwa mwezi Juni mwaka huu, kuziba nafasi ya Bunge la Taifa, limerudia kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwenye nchi hiyo ambayo imeshuhudia ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu kuangushwa kwa utawala wa dikteta Moammer Gaddafi, mwaka 2011.
Ghasia nchini Libya ziliongezeka mwezi Mei baada ya jenerali mstaafu, Khalifa Haftar na wanamgambo wake watiifu kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu kwenye mji wa mashariki wa Benghazi. Mapigano kwenye miji ya Tripoli na Benghazi yamesababisha nchi kadhaa kuwaondoa raia wake pamoja na wanadiplomasia nchini Libya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lapendekeza vikwazo
Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipendekeza kuweka vikwazo kwa wanamgambo wa Libya pamoja na wafuasi wao wa kisiasa, wanaochochea vita vinavyozidi kupamba moto. Naye Balozi wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa, Ibrahim Dabbashi, alionya kuhusu kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya, kama mzozo na mgawanyiko uliopo utaendelea.
Wakati huo huo, wanamgambo wa Kiislamu wanaoudhibiti mju mkuu wa Libya, Tripoli, wamesema wamelikubali pendekezo la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano nchini humo, lakini limeapa kupinga hatua yoyote ya mataifa ya kigeni kuingilia masuala ya Libya.
Kamanda mwandamizi wa kundi hilo, Ahmed Hadiyah amesema kundi lake litashirikiana na jumuiya ya kimataifa, bila ya uhuru wa Libya kukiukwa. Kauli hiyo iliyotolewa jana usiku, inaonekana kama inapinga wito uliotolewa hivi karibuni na wabunge wa Libya, wa kuutaka Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwa lengo la kuzuia mapigano yanayoendelea kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE,RTRE,AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu