Serikali ya mpito Sudan yakutana na viongozi wa waasi
2 Septemba 2020Makamanda wa waasi wa kundi la Sudan Revolutionary Front (SRF) na serikali ya mpito ya Sudan mjini Khartoum walikutana Jumanne katika mazungumzo ya ana kwa ana,hiyo ikiwa ni siku moja baada ya makubaliano ya amani kutiwa saini.
Shirika la habari la taifa SUNA lililoripoti habari hii, limemnukuu Alhadi Idris ambaye ni kiongozi wa muungano huo wa waasi SRF akisema kwamba mkutano huo wa pamoja ni wa kwanza kufanyika baada ya kutiwa saini makubaliano na kilichojadiliwa ni kile kitakachofanyika kuelekea mbele.
Lakini pia kiongozi huyo wa waasi amesema bado kuna masuala kadhaa hayajatatuliwa yanayohusu kipindi cha utekelezaji wa makubaliano.
Kundi la SRF hasa linajumuisha kina nani.
Kundi hili la waasi ni muungano wa makundi matano ya waasi pamoja na makundi manne ya kisiasa,kutoka jimbo la Magharibi la Darfur ,na majimbo ya Kusini ya Kordofan na Blue Nile na liliundwa mwaka 2011.
Kiongozi wa kundi la vuguvugu la Ukombozi wa Sudan yaani SLM la kutoka jimbo la Darfur Minni Minawi,ambalo nalo ni sehemu ya muungano huo,anasema vipaumbele vyao hivi sasa ni maendeleo ya kiuchumi na masuala ya kiutu yanayowahusu watu walioachwa bila makaazi kufuatia migogoro ya Sudan.
Makubaliano ya amani yaliyotiwa saini Jumatatu yanagusia masuala mengi yanayojumuisha usalama,umiliki wa ardhi,utekelezaji wa haki katika kipindi cha mpito,ugawanaji madaraka pamoja na kutolewa nafasi ya watu waliokimbia wakati wa vita kurudi majumbani mwao.
Makubaliano hayo yanagusia pia suala zima la kuvunjwa kwa makundi ya waasi na kujumuishwa wapiganaji katika jeshi la taifa.
Ibainike hapa, kwamba serikali ya mpito ya Sudan mjini Khartoum,iliyoingia madarakani baada ya kuondolewa kiongozi mwenye msimamo mkali Omar Al Bashir Aprili 2019,imelifanya suala la kutafuta amani na makundi ya waasi kuwa kipaumbele chake cha mwanzo kabisa.
Pia ikumbukwe kwamba waasi wa Sudan kwa kiwango kikubwa ni watu kutoka jamii za wasiokuwa waarabu ambao kwa muda mrefu wakiipinga serikali iliyohodhiwa na waarabu mjini Khartoum chini ya bwana Bashir.
Sasa waziri mkuu Abdalla Hamdok anasema kwamba makubaliano ya amani yaliyofikiwa yanajenga dola jipya la Sudan na dawa mujarabu ya ukosefu wa haki uliofanyika huko nyuma.Jana Jumanne akitoa tamko hilo pia aliwayatolea mwito makundi mengine mawili ya waasi yaliyokataa kushiriki kwenye makubaliano hayo.