Serikali ya mpito ya Tunisia mashakani
19 Januari 2011Serikali ya umoja wa taifa nchini Tunisia inatazamiwa kukutana kwa mara ya kwanza kesho-lakini tayari serikali hiyo inazongwa na matatizo baada ya mawaziri wa upande wa upinzani kushikilia serikali ya mpito isiwajumumishe wafuasi wa chama tawala cha zamani-RCD.
Mkutano huo wa kwanza wa baraza la mawaziri ulikuwa ufanyike leo,lakini umeakhirishwa hadi kesho kufuatia malalamiko ya umma dhidi ya kuendelea kuwepo madarakani mawaziri wa mambo ya nchi za nje,mambo ya ndani,ulinzi na fedha .
Mawaziri wanne walijiuzulu jana wakilalamika dhidi ya kuwepo serikalini wafuasi wa Kongamano la katiba kwaajili ya demokrasia-RCD-chama cha rais aliyetimuliwa madarakani Zine Abidin Ben Ali.
Maandamano ya umma yaliyoanza upya jana yanatazamiwa kuendelea leo mjini Tunis na katika maeneo mengine ya nchi hiyo kupinga kushirikishwa serikalini wafuasi wa chama cha RCD.
Tayeb Ben Aicha,ambae ni mwanaharakati wa chama kikuu cha wafanyakazi UGTT anasema
"Hatutaki washiriki serikalini kwasababu tunataka chama tawala cha zamani kivunjwe."
Rais wa mpito Fouad Mebazaa na waziri mkuu Mohammad Ghannouchi wametangaza kujitoa katika chama tawala cha zamani.
Uamuzi huo umetuliza kidogo ghadhabu za baadhi ya wanachama wa upande wa upinzani-hata hivyo chama kikuu cha wafanyakazi UGTT kinasema hautoshi.
Waziri mkuu Ghannouchi anasema baadhi ya mawaziri wanahitajika ili kudhamini kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu utakaoitishwa miezi miwili kutoka sasa.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amewatolea mwito viongozi wa Tunisia "wawajumuishe wawakilishi wa pande zote katika meza ya majadiliano" ili kuunda serikali ya mpito kabla ya uchaguzi mkuu.
Sawa na Tunisia,waarabu wa nchi kadhaa wamechoshwa na kupandishwa bei za vitu,umaskini,ukosefu wa ajira na utawala wa kimabavu-hali iliyopelekea mtu mwengine kujitia moto nchini Misri hapo jana.
Warabu wengi wanayaangalia "mapinduzi ya Tunisia" kama mfano wa kuigizwa ili kuondokana na woga wa wananchi wanaozidi kukandamizwa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters
Mpitiaji:Abdul-Rahman