1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Serikali Ujerumani yakubaliana kuhusu bajeti ya 2024

13 Desemba 2023

Baada ya majadiliano ya mvutano hatimae serikali ya Ujerumani,imeafikiana kuhusu njia ya kujaza pengo la Euro takriban bilioni 17 katika bajeti yake ya mwaka 2024

Deutschland, Berlin | Olaf Scholz, Robert Habeck und ChristianLindner
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Serikali ya mseto nchini Ujerumani,ikiongozwa na Kansela Olaf Scholz imefikia makubaliano ya kuondowa mkwamo wa bajeti. Makubaliano hayo bado hayajatangazwa rasmi ingawa chanzo rasmi kilichozungumza na shirika la habari la AFP leo Jumatano kimesema tamko na ufafanuzi wa kina litatangazwa baadae.

Hatimae dakika za mwisho serikali ya mseto ya chama cha Social Democratic SPD, Kijani na Free Democratic, FDP inaelezwa kwamba imefikia makubaliano ya kuepusha mkwamo wa bajeti uliosababishwa na hatua ya mahakama ya katiba ya kuzuia mipango wa matumizi ya serikali.

Serikali ya Ujerumani ilikuwa kwenye mgogoro mkubwa kuhusiana na suala hilo na kufikiwa kwa makubaliano inamaanisha kwamba msuguano ndani ya serikali utapunguwa na huenda ikawa hatua itakayowapa uhakika wafanyabiashara katika nchi hii kubwa kiuchumi barani Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akihutubia bungeni kuhusu hali ya bajeti,mwezi Novemba 28.2024Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Chanzo kilichozungumza na shirika la habari la AFP, hakikutowa maelezo kuhusu zitakakopatikana takriban yuro bilioni 17 kujaza pengo la bajeti lakini kwa mujibu wa serikali ni  kwamba Kansela Scholz,waziri wa fedha Christian Lindner wa FDP na waziri wa uchumi Robert Habeck kutoka chama cha Kijani watatoa taarifa baadae mchana huu katika ofisi ya Kansela.

Soma pia: Scholz alihutubia bunge la Ujerumani kuhusu mgogoro wa bajetiBila shaka hatua ya kufikiwa makubaliano ilikuwa inasubiriwa kwa hamu nchini Ujerumani,japokuwa pia ni wazi hivi sasa  kwa namna yoyote ni kwamba  bunge mjini Berlin halitofanikiwa kukamilisha mwaka huu mchakato wa kuipitisha  bajeti ya mwaka 2024.

Mgogoro wa bajeti katika serikali ya Ujerumani umekuja katika wakati ambapo uchumi wa nchi tayari ulikuwa katika hali ya kujikongoja na umezusha khofu kwamba ruzuku kubwa zinazozowavutia wawekezaji wakigeni huenda zikaondolewa,na kuchelewesha mipango muhimu ya nchi ya kutaka kuachana na mifumo ya uzalishaji inayochafua mazingira.

Kilichosababisha msuguano

Waziri wa fedha Christian Lindner akiwakilisha mipango ya bajeti mnamo mwezi Septemba Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Msuguano mkubwa uliokuwepo kati ya wanachama wa serikali ya mseto ya vyama vitatu unahusiana  na sheria ya ukomo wa ukopaji wa serikali iliyojumuishwa kwenye katiba ya nchi mwaka 2009,na ambayo inaizuia serikali kukopa zaidi ya asilimia 0.35 ya pato jumla la nchi kwa mwaka kwaajilio ya kuziba pengo la nakisi yake ya bajeti,isipokuwa tu pale panapotokea hali ya dharura. Mara hii serikali mjini Berlin ilitaka kutumia fedha zilizobakia kwenye mfuko wa kushughulikia janga la Uviko,katika miradi yake ya mazingira na viwanda.

Kwa kuzingatia sheria hiyo hiyo ya mwaka 2009 mahakama ya Katiba ikaizuia serikali kuchukuwa hatua hiyo.Na uamuzi huo wa Mahakama ukasababisha kuwepo pengo kubwa la bajeti ya matumizi ya serikali hali iliyoilazima serikali hiyo ya Kansela Scholz kupitisha bajeti ya dharura kwa mwaka huu wa 2023 na kuifanya kutumbukia katika hali ya kusaka namna nyingine mpya  ya kukamilisha bajeti ya mwaka ujao.

Wakati idadi ya wazee ikizidi kuongezeka  nchini Ujerumani wahafidhina wamekuwa wakitoa hoja kwamba  sio sawa kuwaongezea mzigo kizazi cha vijana kwa hatua ya kuendelea kukopa. Kwa mujibu wa waziri wa fedha Christian Lindner  serikali inahitaji hadi yuro bilioni 17 kulijaza pengo la bajeti ya mwaka 2024.