1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya muungano wa vyama vikuu GroKo Magazetini

Oumilkheir Hamidou
23 Januari 2018

Kizungumkuti cha makubaliano ya kuanzishwa mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu, GroKo kati ya CDU/CSU na SPD, makubaliano ya Urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani na mzozo wa Katalonia Magazetini

Nie Wieder Groko Button mit Zeitung
Picha: DW/K. Brady

 

Tunaanzia Berlin ambako mabishano yamepamba moto ndani ya chama cha Social Demorat SPD kati ya wanaounga mkono na wale wanaopinga fikra ya kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu au Groko kama inavyoitwa. SPD wanatiwa kishindo pia na vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU, anasema mhariri wa gazeti la "Schwäbische Zeitung". "CDU/CSU wanataka kukorofisha azma ya SPD ya kudurusiwa makubaliano yaliyofikiwa. CDU na CSU wanabidi waregeze kamba ikiwa wanataka serikali iundwe  na iongozwe na Angela Merkel. Isingekuwa shida kwa CDU/CSU kuridhia kwa mfano katika suala la kuondolewa vikomo katika mikataba ya kazi. Na hata katika suala la familia za wakimbizi kuungana na watoto wao, CDU/CDU wanaweza kuwaridhisha SPD , pindi mada tete zikijadiliwa upya. Lakini nao wana SPD watambue hawana nafasi yoyote ya kukubaliwa madai yao kuhusu mishahara sawa kwa madaktari wa kujitegemea na wale wa serikali, kwasababu tayari madai yao ya kutaka malipo sawa katika bima ya afya  kati ya muajiri na muajiriwa yameshakubaliwa. Inakadiriwa kwamba Angela Merkel anayazingatia yote hayo kama fidia ya kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu. Wahafidhina wa CDU/CSU ambao kwasasa wana maoni tofauti, watalazimika kuungama."

Miaka 55 ya Mkataba wa Elysée kati ya Ujerumani na Ufaransa

Ujerumani na Ufaransa wameadhimisha miaka 55 jana tangu kansela wa zamani Konrad Adenauer na rais wa wakati ule wa Ufaransa Charles de Gaulle walipokutana katika kasri la rais mjini Paris, Elysée na kutiliana saini makubaliano ya urafiki kati ya nchi mbili baada ya miaka kadhaa ya uhasama. Miaka 55 baadae makubaliano hayo ya Elysée kama yanavyoitwa, yanabidi yafanyiwe marekebisho, anasema mhariri wa gazeti la "Rheinpfalz". "Katika historia ya kuliunganisha bara la ulaya daima juhudi zimekuwa zikifanyika kusaka nguvu mbadala inayoweza kukamata nafasi ya injini ya Ujerumani na Ufaransa. Lakini kila mara imedhihirika kwamba Umoja wa Ulaya unaihitaji injini hiyo ili kusonga mbele, na leo hii injini hiyo inahitajika zaidi kuliko wakati wowote mwengine. Injini hiyo inajipatia nguvu zake kutokana na tofauti zilizoko katika nchi hizo mbili. Mpaka sasa miundo mbinu ya nchi hizo mbili, mfumo wao wa kiuchumi na pia mijadala katika jamii inabainisha wazi wazi tofauti zilizoko kati ya nchi hizo mbili. Lakini badala ya kupalilia tofauti na uhasama wa miongo na karne kadhaa nchi hizo mbili zinashadidia umuhimu wa kuzitumia tofauti zilizopo katika kuimarisha jamii ya wajerumani na wafaransa wanaojifunza pamoja na kufaidika kwa namna moja sawa na utakavyofaidika umoja wa ulaya kwa jumla."

Mzozo wa Katalonia unabidi kufumbuliwa

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka Uhispania na kumulika mzozo wa jimbo linalopigania kujitrnga la Katalonhia. Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaandika: "Kizaazaa cha Katalonia kinaendelea. Serikali ya mjini Madrid inabidi iregeze kamba na kutoa mapendekezo. Pengine kuhusu utawala mkuwa zaidi wa ndani. Na hilo linabidi lijadiliwe. Pengine Carles Puigdemont si mshirika anaefaa mazungumzoni.Tangazo lake la upande mmoja la uhuru limemponza rais huyo wa zamani wa jimbo la Katalonia. Pengine kiongozi mwengine anabidi achaguliwe. Kwa vyovyote vile lakini madai ya uhuru wa Katalonia wanabidi waachane nayo."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW