1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya AfD ni "adhabu" kwa serikali ya Scholz?

2 Septemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameyataja matokeo ya uchaguzi katika majimbo mawili ya Saxony na Thuringia yaliyokipatia ushindi mkubwa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD kuwa yanayoumiza.

Ujerumani| Viongozi wa serikali ya muungano Habeck-Scholz -Lindner
(Kutoka kushoto-Kulia) Waziri wa Uchumi na Ulinzi wa Mazingira wa Ujerumani Robert Habeck, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri wa Fedha Christian LindnerPicha: TOBIAS SCHWARZ/AFP/Getty Images

Uchaguzi wa majimbo nchini Ujerumani una maana kubwa zaidi kwa siasa za kikanda. Unatazamwa kama kipimo cha utendajikazi wa serikali ya shirikisho. Licha ya kwamba ni majimbo mawili kati ya 16 ya Ujerumani yaliyopiga kura Septemba Mosi kwa wapiga kura milioni 5 kati ya milioni 61 wa nchi nzima, matokeo yake yana umuhimu mkubwa.

Hii ni mara ya kwanza katika uchaguzi wa bunge wa jimbo ambao chama cha mrengo mkali wa kulia kikijiita chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD kimejizolea zaidi ya theluthi moja ya kura. Kwa nyongeza tu ni kwamba, vyama vinavyounda serikali ya shirikisho ya Ujerumani havijawahi kushuhudia matokeo mabaya zaidi ya kikanda.

Katika majimbo ya mashariki ya Saxony na Thuringia, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD kilipata kura mara mbili zaidi ya vyama vitatu vinavyounda serikali ya mseto ya shirikisho, Social Democrats SPD, chama cha wanamazingira cha Greens na kile cha Free Democrats FDP kwa pamoja. Chama cha kijani cha The Greens na FDP katika majimbo yote mawili vimeshindwa kupata asilimia 5 ili kuwa na uwakilishi kwenye mabunge ya jimbo. Kiongozi wa AfD huko Thuringia Bjoern Hoecke ameyataja matokeo hayo kuwa ya kihistoria. Soma Pia. Wapiga kura katika majimbo 2 ya mashariki mwa Ujerumani wanapiga kura katika uchaguzi muhimu

"Sisi ndio wenye nguvu zaidi. Sisi ndio chama kipya cha watu wa Thuringia, huo ni ushindi wa kihistoria kwetu na kinachonifanya nijivunie pia ni kwamba sisi kama AfD Thuringia, ni chama cha kwanza cha majimbo kupata ushindi huu mzuri wa ubunge wa AfD, kwa chama kichanga na kushinda uchaguzi wa ubunge," alisema Hoecke.

Uungwaji mkono wa AfD mashariki mwa Ujerumani

03:05

This browser does not support the video element.

Matokeo ni "adhabu" kwa serikali ya Berlin?

Chama cha SPD ambacho ni sehemu ya serikali ya mseto nacho kilikuwa katika kitisho cha kutupwa nje ya bunje la jimbo, kulingana na kura za maoni za kabla ya uchaguzi, lakini mwishowe kimesalimika.

Wapiga kura wanne kati ya watano wa Ujerumani walisema kuwa hawaridhiki na utendaji kazi wa serikali ya shirikisho na hilo limekuwa hivyo kwa muda. Utafiti wa kila mwezi wa wapiga kura unaonyesha matokeo mabaya kwa Kansela Scholz na mawaziri wake.

Muungano huo unaonekana mara kwa mara kujiingiza katika mivutano na kushindwa kuchukua hatua. Hata namna serikali ilivyoshughulikia na kwa kauli moja shambulio baya la kisu huko Solingen, magharibi mwa Ujerumani, muda mfupi kabla ya uchaguzi imeshindwa kubadili matokeo.

Robert Habeck, Annalena Baerbock, Olaf Scholz, na Christian LindnerPicha: Chris Emil Janßen/imago images

Kwa kuutupia macho mjadala wa uhamiaji wakati wa kampeni za uchaguzi, serikali ya shirikisho wiki iliyopita ilitangaza sera kali za uhamiaji na usalama, na kuchukua hatua ya kushangaza ya kuwafukuza waomba hifadhi 28 ambao walikuwa wamefanya makosa ya jinai na kuwarejesha Afghanistan.

Macho yote ni huko Brandenburg

Baada ya matokeo hayo, sasa macho yote yanaelekezwa huko Mashariki katika jimbo la Brandenburg ambako kutafanyika uchaguzi mnamo Septemba 22. Huko pia, chama cha AfD kinaongoza katika kura za maoni, kikifuatiwa kwa karibu na Social Democrats. SPD watafanya kila linalowezekana ili kusalia watulivu kuelekea uchaguzi huo, kwasababu utakuwa muhimu kwao.

SPD imeongoza serikali katika jimbo hilo la Brandenburg tangu mwaka 1990. Kiongozi mwenza wa SPD Lars Klingbeil alisema mjini Berlin kwamba anatumai "kila mmoja atafanya juhudi zaidi kuliko hapo awali". Chama hicho kina jukumu la kufanya kazi kwa pamoja kuwashawishi tena wapiga kura.Ujerumani: AfD ya mrengo wa kulia yatafuta mafanikio katika kura ya Saxony, Thuringia

Licha ya matokeo mabaya huko Thuringia na Saxony, Kansela Scholz anaweza kuendelea kuungwa mkono na chama chake. Uongozi wa SPD umesisitiza kuwa Scholz atakiongoza chama hicho katika uchaguzi ujao wa shirikisho.

Ari hii ya mshikamano inaweza kusambaratika haraka iwapo waziri mkuu wa jimbo la Brandenburg aliyedumu kwa miaka 11, Dietmar Woidke, atashindwa kuchaguliwa tena. Katika hali hii uvumi ndani ya SPD unaweza kuenea zaidi kwamba Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius, ambaye ni maarufu zaidi kuliko Scholz, anaweza kuwa mgombea wa Ukansela katika uchaguzi wa shirikisho mnamo Septemba mwaka 2025.

Kiongozi wa AfD Thuringia Björn HöckePicha: Daniel Vogl/dpa/picture alliance

Changamoto kwa serikali ya muungano

Je, muungano wa SPD, chama cha kijani na kile cha FDP utadumu hadi lini? Katibu wa SPD, Kevin Kuhnert alisema kuwa "sasa litakuwa suala la kuwa huru zaidi na kuweka wazi zaidi kile ambacho kinaweza tu kufikiwa na SPD, na kwamba hatutaruhusu tena vyama vingine kututawala."

Maeneo muhumu yanayoweza kuzua mzozo ni pamoja na bajeti ya mwaka 2025 ambayo ni lazima ipitishwe bungeni.Mkwamo wa bajeti watishia kuivunja serikali ya Ujerumani

Pia itategemea ikiwa serikali itaweza kutekeleza sera zake za uhamiaji zilizoimarishwa hivi karibuni. Baadhi ya sauti muhimu katika muungano huo wa vyama vya mrengo wa kushoto vya SPD na The Greens hazikubaliani na mipango ya kuzuia wahamiaji.

Hakuna chama hata kimoja katika muungano huo wa vyama vitatu ambacho kipo tayari kuona muungano huo ukiporomoka. Kama uchaguzi wa kitaifa ungefanyika mapema, kura za sasa za maoni zinaonyesha kwamba muungano huo usingepata wingi wa kura. Washindi wangekuwa vyama hasimu vya AfD, na muungano wa kihafidhina wa Christian Democrats CDU na chama ndugu cha Bavaria cha Christian Social Union CSU.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW