Senegal yasaka suluhu mzozo wa kuahirisha uchaguzi
16 Februari 2024Akizungumza kwenye mahojiano na redio moja ya kibinafsi nchini humo siku ya Ijumaa (Februari 16), msemaji wa serikali, Abdou Karim Fofana, alisema kwamba serikali imezingatia uamuzi wa Baraza la Katiba, lakini hakufafanua ikiwa hilo linaamisha kwamba ingelikubali maamuzi hayo.
Ofisi ya Rais pia haikusema lolote kuhusu iwapo ingeliuheshimu uamuzi huo.
Soma zaidi: Wabunge wakamatwa wakipinga kuahirishwa uchaguzi Senegal
Wakati huo huo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imetoa wito kwa mamlaka nchini Senegal kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa rais kulingana na uamuzi huo wa Baraza la Katiba, ambao ulisema kuahirishwa kwake kulikuwa kinyume cha katiba.
Umoja wa Ulaya pia umezitaka pande husika nchini Senegal kutii uamuzi huo wa Baraza la Katiba.