Serikali ya Somalia yakataa matokeo ya uchaguzi wa Jubaland
27 Novemba 2024Serikali ya Somalia imesema haitatambua kuchaguliwa tena kwa kiongozi wa eneo la kusini la Jubaland, hatua inayochochea mpasuko na maeneo yenye utawala wao wa ndani.
Bunge la Jubaland siku ya Jumatatu lilipiga kura kumchagua tena Ahmed Madobe, mbabe wa zamani wa kivita aliye madarakani tangu 2012 kama kiongozi wake.
Lakini serikali kuu ya Somalia imesema mchakato huo haukuwa halali kisheria kwa kuwa Madobe hakustahiki kugombea baada ya kutumikia mihula miwili kulingana na katiba.
Msemaji wa serikali Farhan Jimale amesema mwanasheria mkuu ameelekezwa awasilishe kwa haraka mashtaka dhidi ya Madobe katika mahakama ya juu kabisa ya nchi.
Madobe amepuuzilia mbali upinzani kutoka kwa serikali kuu mjini Mogadishu akisema yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutawala Jubaland kwa sasa.