Serikali ya Sudan yavikosoa vikwazo dhidi ya mkuu wa jeshi
17 Januari 2025Wizara ya mambo ya nje ya Sudan inayoungwa mkono na jeshi, imelaani vikwazo vilivyotangazwasiku ya Alhamisi na Marekani dhidi ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, ikisema havina msingi wa haki wala uwazi.
Wizara hiyo imesema kwenye taarifa kwamba vikwazo hivyo vinaleta mkanganyiko baada ya miezi 21 ya vita kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, na kusisitiza kuwa Burhan anawatetea watu wa Sudan dhidi ya kile ilichotaja kama njama ya mauaji ya kimbari.
Siku ya Alhamis, wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya Burhan, ikilishutumu jeshi kwa kushambulia shule, masoko na hospitali na kutumia chakula kama silaha ya vita.
Haya yanajiri wiki moja baada ya Marekani kumuwekea pia vikwazo kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, ikilishutumu kundi lake kwa kufanya mauaji ya halaiki.