1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yazidi kushambulia raia wake

7 Februari 2018

Mashambulizi mapya yaliyofanywa na serikali ya Syria yamesababisha vifo vya raia 23 katika mji unaodhibitiwa na waasi karibu na Damascus ambako watoa huduma wa afya wameelemewa na idadi kubwa ya majeruhi.

Syrien Krieg - Ostghuta bei Damaskus
Picha: Reuters/B. Khabieh

Mashambulizi mapya yaliyofanywa na serikali ya Syria yamesababisha vifo vya raia 23 katika mji unaodhibitiwa na waasi karibu na Damascus ambako watoa huduma wa afya wameelemewa na idadi kubwa ya majeruhi katika siku ambayo imeshuhudia vifo vingi zaidi katika mzozo huo wa Syria.

Eneo la mashariki ya Ghouta, linalodhibitiwa na makundi ya jihadi na makundi ya Kiislamu yenye itikadi kali, jana Jumanne limekabiliwa na mashambulizi makali zaidi tangu mzozo huo ulipoanza, na idadi ya vifo inazidi kuongezeka.  

Mkuu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza Rami Abdel Rahman amesema vifo vya raia vimefikia 80 hadi sasa, baada ya majeruhi wengine wawili kufariki usiku wa jana.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba idadi hii ni kubwa zaidi nchini Syria kwa karibu miezi tisa, na moja ya siku zilizoshuhudia mauaji mengi zaidi mashariki mwa Ghouta kwa miaka mingi.

Hakukua na nafasi ya kupumua kwa raia wa Ghouta, kwa kuwa ndege za kijeshi za serikali zilirejea mapema asubuhi ya leo na kufanya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya raia wengi katika maeneo kadhaa.  

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian(katikati) akiwa kwenye mkutano mjini BrusselsPicha: Reuters/J.Thys

Mapema leo, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alitaka wapiganaji wote wanaoungwa mkono na Iran ambao ni pamoja na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon walioko nchini Syria kuondoka, na kusema kwamba Uturuki na Iran zilikuwa zikikiuka sheria za kimataifa kutokana na hatua zake nchini humo. 

Akizungumza na kituo cha televisheni cha BFM, Waziri huyo ameitaka Uturuki kuacha kuchochea mzozo huo kuwa mbaya zaidi, ingawa hakutoa mwito wa moja kwa moja kwa nchi hiyo kuitaka kuacha mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Syria. 

Alipoulizwa katika mahojiano hayo na kituo hicho cha BFM, kuhusu iwapo angetaka vikosi vya Uturuki kuondoka nchini Syria, Le Drian alisema.

Aidha, amesema zipo ishara kwamba majeshi ya serikali ya Syria yalitumia gesi ya sumu dhidi ya raia, ingawa Umoja wa Mataifa unahitaji kulithibitisha hilo.

Wataalamu wa Uturuki wakiwa wamembeba muhanga wa silaha za sumu katika mji wa Idlib, Syria.Picha: picture alliance/AP Photo

Shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya silaha za kemikali, OPCW kwa upande wake limesema hii leo kwamba linachunguza madai yote ambayo ni ya msingi ya matumizi ya silaha hizo za kemikali nchini Syria, wakati kukiongezeka madai kwamba serikali ya Syria imetumia silaha hizo.

katika hatua nyingine, ndege za kijeshi za Israel zimeshambulia kwa makombora eneo la kijeshi la Syria lililoko karibu na Damascus, ingawa hata hivyo mengi yaliharibiwa na mfumo wa kujikinga na makombora wa Syria. Taarifa hii ni kulingana na kituo cha televisheni cha serikali. 

Msemaji wa jeshi la Israel, mjini Jerusalem kwa upande wake alinukuliwa akisema "hatuwezi kujibu ripoti kama hizo". Ripoti hii ni ya pili kutolewa ikiwa na madai kama hayo dhidi ya Israel katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/RTRE
Mhariri:Iddi Ssessanga
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW