1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania hakuna mapambano kati ya askari na wananchi

10 Juni 2022

Serikali ya Tanzania imesema hakuna mapambano yoyote kati ya askari polisi na wananchi katika kijiji cha Loliondo kama video inavyosambaa mtandaoni inavyoonyesha kuwa kuna mapigano kati ya wanakijiji na askari polisi.

Maasai aus Loliondo in Tansania
Picha: Judith Fehrenbacher

Kauli hiyo ya serikali imetolewa hii leo na waziri mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa bungeni jijini Dodoma, baada ya spika wa bunge Tulia Ackson, kumtaka waziri mkuu kutoa ufafanuzi kuhusiana na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna mapigano kati ya wananchi na askari poilisi katika eneo la Loliondo kaskazini mwa Tanzania.

Waziri mkuu Majaliwa ameongeza kuwa video inayosambaa mtandaoni ilikuwa ni mkakati wa kutengeneza ili kuleta taswira mbaya ndani ya nchi na nje ya nchi na kuongeza kuwa.

soma Maboma ya Wamasai yachomwa Tanzania

"Kimsingi hakuna mapambano yoyote. Hakuna askari aliyekwenda huko kijijini kwenda kutishia kwa namna yoyote ile kwa sababu kwenye mipango yote hakuna kijiji kinaondolewa, hakuna mwananchi anaondoka hakuna tatozo lolote la mifugo. Tuliona tuseme hili ili kuwaondolea Watanzania dhana mbovu dhidi ya serikali kwamba labda serikali inataka kuwaondoa hawa wafugaji, inataka kuvunja vijiji vya wafugaji hasa vijiji hivyo 14 kwenye eneo la Loliondo.

Aidha Waziri mkuu Majaliwa ameongeza kusema kuwa serikali itaweka mipango ya kuratibu vizuri eneo hilo na kwamba likiratibiwa vyema kwa mifugo ya watanzania tu litakuwa chanzo endelevu na likiruhusiwa kuongeza idadi ya ng'ombe kutoka maeneo mengine eneo hilo litapotea.

Tulia ataka ufanunuzi zaidi

Spika wa bunge Dkt. Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Awali spika wa bunge la Tanzania Tulia Ackson kabla ya kuhitimisha mkutano wa leo wa bunge alimtaka waziri mkuu kutolea ufafanuzi video hiyo inayoonyesha kuwa kuna mapigano huko Loliondo kati ya askari na wanakijiji, huku akitaka wale waliotengeneza video hiyo na hivyo kuzua taharuki wachukuliwe hatua haraka za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

"Sisi wabunge tunafahamu na serikali inafahamu kwamba hata wananchi wengine wanaotaka kufahamu pia wanafahamu kwamba tuko kwenye vita ya kiuchumi na nchi zengine. Sasa tukiwaacha hawa wakaendelea kutumika wale waliopo hapa nchini sheria zetu zichukue mkondo wake. Kama mtu anafanya upotoshaji kama huyo ambaye amechuku hiyo clip na inajulikana ameichukulia wapi, Tunaweza kuanza na huyo alafu wengine watakuwa wanafuata ikiwa ni pamoja na hizi taasisi ambazo zimesajiliwa hapa nchini kwetu kama zinafanya jambo tofauti pia sheria zichukue mkondo wake."

Kufuatia kuongezeka kwa idadi ya ng'ombe na watu pamoja shughuli za kijamii katika eneo la Loliondo serikali ya Tanzania imekuwa ikitoa elimu namna ya umuhimu wa kutunza eneo hilo huku ikiendesha zoezi la kuwahamisha wananchi waliojiandikisha kwa hiari yao.

 

Deo Kaji Makomba/DW Dodoma.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW