1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Tanzania yaunda tume na wafanyabiashara

17 Mei 2023

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametangaza kuunda tume ya watu 14 inayowajumuisha maafisa wa serikali na wafanyabiashara kutathmini adha ambazo zimepelekea mgomo wa wauzaji maduka kwenye mitaa ya Kariakoo.

Tansania Dar Es Salaam | Kariakoo Markt | Händler
Picha: Said Khamis/DW

Ilikuwa ni siku refu kwa Waziri Mkuu Majaliwa na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo lililopo kwenye kitovu cha jiji kuu la biashara na uchumi, Dar es Salaam, katika jitihada za kuuzima mgomo wa kufungua maduka ulioanza siku mbili zilizopita.

Wengi miongoni mwa wafanyabiashara waliozungumza kwenye mkutano huo wa wazi walitowa hisia kali dhidi ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchembe, pamoja na Mamlaka ya Mapato (TRA) wakidai ni sehemu ya uanzishwaji wa sheria na kanuni zinazowakandamiza.

Soma zaidi: Wafanyabiashara katika soko la kariakoo, Tanzania walalamikia kunyanyaswa na mamlaka za jiji la Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao walimuambia Waziri Mkuu Majaliwa kwamba Mwigulu na TRA hawawajali wafanyabiashara, wanafuga mianya ya rushwa na wanaanzisha sheria na kanuni kandamizi ambazo si rafiki kwa ufanyaji biashara nchini Tanzania.

Mwigulu 'akaangwa' mbele ya Majaliwa

Wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo.Picha: Said Khamis/DW

Awali wafanyabiashara walianza kukusanyika nyakati za asubuhi wakimsubiri waziri mkuu huyo aliyewasili eneo la Mnazi Mmoja majira ya saa 7:00 mchana na kuendelea kuzungumza nao mpaka majira ya jioni.

Mbali na Waziri Mwigulu na TRA, wafanyabiashara hao walilalamikia urasimu unaofanywa na idara mbalimbali za serikali, vikiwemo vyombo vya usalama, ambapo jeshi la polisi lilijikuta tena likitumbukia katika kashfa ya rushwa huku maafisa wake walilaumiwa kwa kukwamisha shughuli za biashara.

Maafisa wa jeshi hilo walitajwa kuendesha ukaguzi usiokuwa na tija kwa mizigo na bidhaa hata pale mizigo hiyo inapokuwa na stakabadhi zinazotambulika na mamlaka husika.

Serikali yaunda kamati ya watu 14

Wanunuzi kwenye Soko la Kariakoo.Picha: Said Khamis/DW

Akihitimisha mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa alitangaza tume maalumu ya wajumbe 14, saba kutoka serikalini na wengine saba kutoka jumuiya ya wafanyabiashara "watakaokuwa na kazi ya kuzichambua hoja zote zilizowasilishwa na wafanyabiashara wenyewe."

Licha ya kwamba chanzo cha mkutano huo ni mgomo wa wauza maduka katika mitaa ya Soko la Kariakoo ulioanza siku ya Jumatatu (Mei 15), lakini uliwaleta pia viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara kutoka kote nchini waliojadili na kupendekeza namna ya kukwamua hali hiyo.

Kariakoo ni kama kituo kikuu cha biashara za kawaida na za kila siku nchini Tanzania na kwa wengi ni kama soko la kimataifa, kwani linahudumia wafanyabiashara kutoka mataifa jirani kama vile Zambia, Kongo, Burundi na Rwanda.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW