1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Uganda yatakiwa kuimarisha usalama Karamoja

6 Septemba 2021

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Uganda kushughulikia suala la kuzorota kwa usalama katika kanda ya Karamoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Uganda Kaabong Wahlen Karamojong Volk
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mabalozi wa nchi wanachama wa ujumbe huo wana mtazamo kuwa kuongezeka kwa visa vya wizi wa mifugo, mauaji, utekaji nyara wa wanawake na uvamizi wa watu waliojihami kwa bunduki ni miongoni mwa uhalifu ulioshamiri katika eneo hilo katika siku chache zilizopita. 

Kisa cha mifugo wote kuibwa kutoka kijiji kimoja kijulikanacho kama Kakamar ni kielelezo tosha kuwa wizi wa mifugo ambayo ndiyo rasilimali kubwa kwa watu wa jamii ya wafugaji wa kuhamahama wa Karamoja kimefikia kiwango cha kushtusha. Licha ya serikali kuelezea kuwa imeanza kukabiliana na hali hiyo, kila kukicha visa vya aina hii vinatokea katika sehemu mbalimbali za eneo hilo. 

Katika kipindi cha wiki mbili, ng'ombe wapatao 1,300 wamechukuliwa na watu waliojihami kwa silaha za kienyeji pamoja na bunduki. Kulingana na kiongozi wa ujumbe wa Ulaya nchini Uganda Atilio Pacifici, hali hii ya kuzorota kwa usalama inastahili kushughulikiwa kwa dharura. La sivyo mafanikio waliokuwa wamepata watu wa eneo hilo kutokana na misaada mbalimbali kutoka mataifa ya Ulaya hayatakuwa na maana yoyote.

soma zaidi: Watu 200 wauawa eneo la Karamoja tangu mwaka huu uanze

Miongoni mwa misaada iliyowahi kutolewa ili kupunguza makali ya maisha kwa watu wa sehemu hiyo inayokumbwa na ukame kila mara ni bwawa la maji ya mifugo lenye thamani ya Euro milioni 11 zilizotolewa na serikali ya Ujerumani.

Picha: DW/F. Yiga

Lakini kinachositikitisha, ng'ombe wote katika eneo hilo wameibwa ikimaanisha kuwa haliwezi kutumiwa. Balozi wa Ujerumani Mathias Schauer ameelezea kuwa ni muhimu kwa serikali ya Uganda kuwajibikia usalama na misaada inayotolewa kwa watu wa jamii hiyo.

Mabalozi wengine wamesisitiza kuwa mataifa ya Ulaya hayawezi kuingilia kati kutatua suala la usalama wa jamii hiyo, ila Uganda ikishirikiana na mataifa jirani wanastahili kuchukua hatua ya makusudi kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu kuna madai kuwa wavamizi hutokea mataifa jirani ya Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia.

Wajumbe hao wana mtazamo kuwa ukosefu wa usalama kwenye eneo hilo unatatiza hata shughuli za elimu kwani watu wa jamii hiyo wanakosa mazingira mazuri ya kuwaelimisha watoto wao. Kwa upande wake, Msemaji wa Majeshi ya Uganda, Brigedia Flavia Byekwaso amesema wanafanya kila juhudi kukamata bunduki zote ambazo watu wa jamii hiyo wanazificha.

Ila kulingana na wadadisi wa masuala ya kisiasa, ukosefu huu wa usalama ni wa kimakusudi ili kufichia uhalifu wa wizi wa madini ya dhahabu na mengine ambavyo vinapatikana sehemu hiyo.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.