1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ugiriki yasalimika: mkopo njiani

22 Juni 2011

Serikali ya Ugiriki imo mbioni kujaribu kuidhinisha mpango wa kubana matumizi yake, baada ya Waziri Mkuu George Papandreou kuungwa mkono katika kura ya imani iliyopigwa bungeni jana usiku.

Waziri Mkuu wa Ugiriki George PapandreouPicha: dapd

Kuambatana na mpango huo, serikali inatazamia kupunguza matumizi yake, kupandisha kodi na kuuza mali yake ili iweze kupata sehemu ya msaada wa fedha uliokubaliwa na Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF mwaka uliopita.

Ugiriki itakuwa muflis?

Serikali ya Ugiriki imenusurika baada ya kuungwa mkono kwa kura 155  bungeni na hivyo imeruka kiunzi cha mwanzo katika jitahada ya kupata mkopo wa dharura ili isijekufilisika.  Waziri Mkuu Papaendreou aliungwa mkono na wabunge wa chama chake cha Pasok, licha ya wengi wao hapo awali kuukosoa vikali mpango wake wa kubana matumizi ya serikali. Waziri mpya wa fedha Evangelos Venizelos jana usiku aliwaambia wabunge kuwa: "Sisi sio wabaya wa Ulaya. Tuna ari na sasa tunapitia wakati mgumu. Lakini katika historia yetu mara nyingi tumeweza kuudhibiti wakati mgumu. Tutathibitisha kuwa kizazi chetu kitashinda vita hivi."

Waandamanaji wa Ugiriki wanaopinga mpango wa kubana matumiziPicha: AP

Madeni na vita

Hivyo ni vita vya kupambana na madeni; na silaha ni mpango wa kubana matumizi unaozusha mabishano makali nchini humo.

Maelfu ya watu walikusanyika nje ya bunge kuupinga mpango huo wakilalamika kuwa masikini ndio wanaobeba mzigo na sio matajiri. Waandamanaji hao wanahisi kuwa vyama vikuu vilivyo bungeni na hata vyama vya upinzani, haviwakilishi maslahi ya umma huo.

Hata hivyo, serikali ya Papandreou iliyopangwa upya hivi karibuni, inataka kuidhinisha mpango huo bungeni hadi Juni 28, ili iweze kupata mkopo mpya kutoka Umoja wa Ulaya na IMF.

Waziri Mkuu George Papandreou na Waziri wa Fedha Evangelos VenizelosPicha: AP

Mkopo wa IMF

Baadaye baraza la mawaziri litapitisha sheria zinazohitajiwa ili kuweza kuutekeleza mpango huo na hivyo kupata msaada wa Euro bilioni 12 na kujiepusha kufilisika. Hatua za kubana matumizi ni masharti ya kupewa fungu jipya la fedha kutoka jumla ya Euro bilioni 110 zilizokubaliwa na Umoja wa Ulaya na IMF katika mpango mpya wa kupunguza matumizi kwa miaka mitano ijayo.

Bila ya mkopo huo, Ugiriki itaishiwa na fedha zake mwezi ujao na maafisa wa serikali wana hofu kuwa kufilisika kwa Ugiriki kutaathiri pia mfumo wa kiuchumi kote duniani.

Mwandishi: Bormann,Thomas/ZPR/afpe,rtre

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW