1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ujerumani yasambaratika

7 Novemba 2024

Naibu kansela Robert Habeck amesema kuwa serikali bado inaweza kuendelea kufanya kazi hata baada ya Kansela Olaf Scholz kumfuta kazi waziri wake wa fedha Christian Lindner wa chama cha sera za kibiashara cha FDP.

Kansela Olaf Scholz
Upinzani Ujerumani unamtaka Kansela Scholz aitishe uchaguzi wa mapema haraka iwezekanavyoPicha: Hannes P. Albert/dpa/picture alliance

Muungano tawala wa Ujerumani ulisambaratika baada ya miaka mingi ya misuguano kufikia kilele chake kuhusiana na sera ya kiuchumi na bajeti katika taifa hilo kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya. Hayo yalijiri muda mfupi tu baada ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa rais Marekani.

Soma pia: Upinzani nchini Ujerumani washinikiza uchaguzi wa mapema

Scholz, wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto – Social Democratic - SPD amesema yeye na chama cha Kijani walitaka kuondoa ukomo wa serikali kukopa ili kuongeza msaada wake kwa Ukraine na kwa uchumi unaoyumba, kitu ambacho waziri wake wa fedha wa chama cha Free Democratic – FDP kinachoegemea sera za kibiashara, Lindner alikipinga. "Mara nyingi, Waziri Lindner amezuia kupitishwa sheria kwa njia isiyofaa. Mara nyingi amejihusisha na mbinu za kipuzi za siasa za vyama. Mara nyingi sana amevunja uaminifu wangu. Hata wakati mmoja alijiondoa kwenye makubaliano ya bajeti wakati tulikuwa tayari tumekubaliana baada ya mazungumzo marefu. Kazi muhimu ya serikali haiwezi kufanyika kwa njia hii."

Kansela Olaf Scholz amekuwa na tofauti za wazi wazi na waziri wake wa fedha Christian LindnerPicha: CHRISTOF STACHE/AFP

Kansela Scholz alisema bado anapanga kupitisha miswada hiyo kabla ya kuandaa kura ya Imani na serikali Januari 15 mwaka ujao ambayo kuna uwezekano atashindwa, na hivyo kuitisha uchaguzi mpya ifikapo mwishoni mwa Machi.

Scholz alitangaza kuwa atamuomba kiongozi wa kundi kubwa kabisa la upinzani Bungeni – Friedrich Merz kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia Christian Democratic Union – CDU, kujadili mbinu za kuimarisha uchumi na ulinzi na kupitisha miswada muhimu bungeni.

Soma pia: Vyama vya serikali ya muungano Ujerumani vyakutana kujaribu kutatua mgogoro

Lakini Merz amekanusha vikali mpango wa Scholz akisema hakuna muda wa kupoteza. "Hakuna sababu kabisa ya kusubiri hadi Januari mwakani. Muungano huo hauna tena wingi wa viti katika Bundestag. Kwa hiyo ni lazima tumuombe Kansela, kwa uamuzi wa pamoja wa kundi la CDU-CSU katika Bundestag, kuandaa kura ya imani sasa. Ikiwezekana ifanyike mapema wiki ijayo."

Naibu Kansela Habeck, ambaye pia ni Waziri wa uchumi, amewaomba raia kuwa na Imani na demokrasia ya nchi, licha ya mgogoro unaoendelea wa kisiasa.

Naibu Kansela Habeck amewataka Wajerumani kuwa na imani na demokrasia ya nchi licha ya mgogoro wa kisiasaPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Upinzani waitisha kura ya haraka ya imani

Wanasiasa kadhaa wa upinzani wamemtaka Scholz kuandaa haraka kura ya imani na serikali badala ya kusubiri hadi Katikati ya Januari kama anavyopendekeza. Mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Christian Social Union – CSU Markus Söder ni miongoni mwa wanaotaka hatua ya haraka.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD kimeita kusambaratika kwa muungano tawala kuwa ni "ukombozi”. Naye Waziri wa Uchukuzi Volker Wissing ameamua kujiondoa katika chama cha FDP, badala ya kujiondoa katika serikali ya muungano. Uamuzi wake ulifuatia tangazo la FDP kuwa litawaondoa wanachama wake kutoka muungano tawala wa Scholz. Wissing amesema leo kuwa Scholz alimuomba aendelee katika wadhifa wake. Waziri wa Elimu Bettina Stark-Watzinger na Waziri wa Sheria Marco Buschmann kutoka FDP wanatarajiwa kuwasilisha rasmi barua zao za kujiuzulu kwa Rais Frank-Walter Steinmeier baadaye leo.

afp, dpa, reuters, ap

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW