1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya umoja nchini Pakistan yaelekea kusambaratika

Kalyango Siraj13 Mei 2008

Mawaziri tisa wajiuzulu kuhusu majaji waliofutwa kazi na Musharraf

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif akihutubia waandishi habari. Chama chake kimejiondoa kutoka serikali ya Umoja kupinga kutowarejesha kazini majaji waliofutwa kazi na rais MusharrafPicha: AP

Serikali ya muungano ya Pakistan ilioundwa wiki sita zilizopita iko mashakani kufuatia kujiuzulu kwa mawaziri kutoka chama cha waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Nawaz Sharif.

Hatua ya mawaziri hao imefuatia uamuzi wa Nawaz kuwaondoa kutoka serikali ya sasa ili kupinga kutotimiza ahadi ya kuwarejesha tena kazini majaji waliofutwa kazi na mpinzani wake mkuu kisiasa rais Perves Musharraf.

Licha ya mawaziri hao tisa kuwasilisha barua za kujiuzulu kwao lakini ofisi ya Waziri mkuu Yousuf Raza Gilani imesema kuwa waziri mkuu hakukubali kujiuzulu kwao haraka akisubiri mkutano na kiongozi wa chama chake Ali Zardari kutoka safari ya nje.Anategemewa kurejea baadae jumanne.

Na ikiwa chama cha Nawaz kitajiondoa katika serikali hiyo,bila shaka hii inaweza ikaifanya serikali ya waziri mkuu kusambaratika.

Nawaz aliamua jumatatu kuwaondoa mawaziri wake kutoka serikali ya muungano baada ya kutofautiana kuhusu suala la majaji.

Majaji waliofutwa kazi walionekana kama wapinzani wa juhudi za rais Musharraf za kuendelea kuwa madarakani .

Na upinzani baada ya kushinda uchaguzi wa bunge juzi inaonekana kana ulikubaliana kuwarejesha kazini majaji hao.Lakini hadi sasa jambo hilo halijafanyika na ndio sababu mojawapo inamfanya Nawaz kuwaondoa mawaziri wake kutoka serikali ya umoja.

Waziri mkuu kwa upande wake anajaribu juhudi za mwishomwisho kuweza kuinusuru serikali yake isisambaratike.Miongoni mwa hatua hizo ni kuchelewesha kukubali kujiuzulu kwa mawaziri wake.

Nao mawakili wa Pakistan wanapanga kufanya maandamano wakitaka serikali kurejesha kazini mara moja majaji hao.

Mmoja wa wanaopanga maandamano hayo Munir Malik amewambia wandishi habari mjini Hong Kong kuwa viongozi wa chama cha mawakili wa Pakistan watakutana jumamosi ili kukamilisha mikakati yao ya maandamano hayo.

Ameongeza kuwa huenda maandamano hayo yakatanguliwa na mkutano wao mjini Lahore na baadae kuandamana hadi majengo ya bunge katika mji mkuu wa Islamabad.Hata hivyo hakutoa tarehe ya maandamano hayo.

Ameongeza kuwa mawakili watakuwa waangalifu ili kutochochea jeshi kuingilia kati likitumia maandamano hayo kama kisingizio.

Kwa mda huohuo mme wa waziri mkuu wa zamani alieuliwa nchini Pakistan Benazir Bhutto,amefutiwa mashataka ya magendo ya vifaa vya kale.Wakili wake amesema kuwa korti ya Pakistan imefuta mashtaka hayo.

Asif Ali Zardari alituhumiwa kwa kujaribu kupeleka nje kimagendo vitu vya kale vyenye thamani kama vile bunduki pamoja na mapanga katika kesi iliofunguliwa mwaka wa 1997 punde tu baada ya mkewe kuondolewa madarakani.

Wakili wake anasema kuwa sasa amebakiza kesi moja tu.