Serikali ya Uturuki imetoa karipio kali kwa balozi za kigeni
3 Februari 2023Vitisho hivyo vilitolewa kufuatia matukio ya kuchomwa kwa Qur-an takatifu kwenye maandamano ya nje kupinga sera ya Ankara kuelekea upanuzi wa jumuiya ya NATO.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema baada ya kumuita balozi wa Ujerumani kwamba ikiwa mataifa hayo yanataka kutoa taswira kwamba Uturuki haina utulivu na kuna hatari ya ugaidi, hilo linakweda kinyume na moyo wa urafiki na ushirikiano.
"Haijalishi namna unavyoitazama hali hii, taarifa hizi na hatua za kufunga balozi ni za kukusudia. Tumetoa onyo zinazohitajika, ikiwa wataendeleza mbinu kama hizo bila kutupatia taarifa thabiti na nyaraka, tutachukuwa hatua stahiki. Tumefikisha ujumbe huu kwao jana," amesema Mevlut Cavusoglu
Wawakilishi wa kidiplomasia wa Marekani, Uholanzi, Sweden, Uwisi, Uingereza, Ubelgiji, Ufaransa na Italia waliitwa pia katika wizara ya mambo ya nje ya Uturuki mjini Ankara kutoa maelezo, baada ya balozi kadhaa kutoa onyo wiki iliyopita, kuhusu ongezeko la kitisho cha mashambulizi nchini Uturuki, na kufunga baadhi ya balozi zao mapema wiki hii.