1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Yemen yakomboa jimbo la kusini

11 Januari 2022

Mafisa wa serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa imesema vikosi vya serikali hiyo vimekomboa jimbo lote la Shabwa Kusini mwa nchi hiyo kutoka kwa waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Maeen Abdul Malek Saeed | jemenitischer Premierminister
Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Serikali, ikisaidiwa na washirika kutoka kwa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, Vikosi vya Giants Brigade na mashambulizi ya angani kutoka kwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ilivamia eneo hilo la Shabwa mwezi huu na kulikomboa jimbo hilo lote katika mapigano ya siku 10. Msemaji wa jeshi Mohammed al-Naqib, amesema wamefanikiwa kukomboa maeneo yote yaliolengwa na kuwafurusha waasi hao wa Kihouthi kutoka wilaya za Ain, Usailan na Bayhan.

Gavana akiri kukombolewa kwa Shabwa

Gavana Awad al-Awlaki pia alitangaza kukombolewa kwa Shabwa na kuishukuru Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilizofadhili muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia unaopigana na waasi hao wa Kihouthi. Hakukuwa na tamko la mara moja kutoka kwa Wahouthi lakini viongozi wawili waasi waliozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, walikiri kwa shirika la habari la Associated Press kwamba wamepoteza uthibiti wa Shabwa. Viongozi hao wameongeza kuwa waasi hao walitorokea mikoa ya karibu ya Bayda na Marib.

Waasi wa KihouthiPicha: Mohammed Hamoud/NurPhoto/picture alliance

Kukombolewa kwa eneo la Shabwa, kutaviwezesha vikosi vya serikali kufunga njia kuu za usambazaji bidhaa kwa waasi hao ambao wamekuwa wakishambulia mji huo muhimu wa Marib ambao ni ngome ya mwisho ya serikali katika eneo la Kaskazini mwa Yemen tangu mapema mwaka jana. Mara kwa mara, waasi hao wametatiza juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Mataifa na Marekani za kusitisha mashambulizi ya Marib pamoja na mashambulizi ya waasi ya roketi na ndege zisizo na rubani dhidi ya Saudi Arabia.

Juhudi za mazungumzo zagonga mwamba

Juhudi za mazungumzo zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa zimeshindwa kupata ufanisi katika mzozo huo wa miaka kadhaa nchini Yemen. Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mnamo mwaka 2014 wakati Wahouthi walipochukuwa uthibiti wa mji mkuu wa Sanaa na eneo kubwa la Kaskazini mwa Yemen na kuilazimu serikali kukimbilia upande wa Kusini, na baadaye uhamishoni nchini Saudi Arabia. Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao wakati huo uliungwa mkono na Marekani, uliingia katika miezi ya vita baadaye ukijaribu kudumisha ushawishi wa serikali.

Vita hivyo kwasasa vimesababisha vifo vya maelfu ya raia na wapiganaji. Vita hivyo pia vimesababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu na kuwaacha mamilioni ya watu wakitaabika kutokana na uhaba wa chakula na dawa na kutishia kulitumbukiza taifa hilo katika baa la njaa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW