1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Shambulio dhidi ya hospitali ya wazazi laua kichanga Ukraine

23 Novemba 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameituhumu Urusi kuleta ugaidi na mauaji nchini Ukraine, baada ya shambulio dhidi ya wodi ya wazazi kuuwa kichanga katika mkoa wa kusini wa Zaporizhzhia.

Ukraine Mariopol | Zerstörung nach Russischen Angriff auf Krankenhaus
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Waokoaji wamesema kupitia mitandao ya kijamii kuwa mtoto huyo mchanga ameuawa usiku wa kuamkia leo, kufuatia shambulio la roketi dhidi ya hospitali katika mji wa Vilniansk katika mkoa wa Zaporizhzhia, ambapo jengo la ghorofa mbili la wodi ya wazazi liliharibiwa.

Mama wa mtoto huyo na daktari waliondolewa wakiwa hai. Gavana wa mkoa huo alisema roketi zilizofyatuliwa ziliwa za Urusi.

Soma pia: Zelensky: Urusi imeshambulia hospitali na vituo vya matibabu

Shambulio hilo linaongezea kwenye mateso yalioshuhudiwa na hospitali na vituo vingine vingine vya matibabu--na wagonjwa wao na wafanyakazi--katika uvamizi wa Urusi unaoingia  mwezi wake wa tisa wiki hii.

Wamekuwa wakilengwa tangia mwanzo mwa uvamizi huo, ikiwemo shambulizi la Machi 9 lililoharibu hospitali ya wazazi katika mji wa bandari ambao kwa sasa unakaliwa na Urusi wa Mariupol.

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Valentyn Ogirenk/REUTERS

Rais Volodymyr Zelenskiy, amesema "kwa mara nyingine adui amejaribu kufanikisha kwa ugaidi na mauaji, kile alichoshindwa kufanikisha kwa miezi tisa na ambacho hatoweza kukifanikisha."

Badala yake, ameongeza kupitia mtandao wa kijamii, kwamba nchi hiyo itawajibishwa tu kwa uovu wote iliyouleta Ukraine.

Ukraine yaunda "vituo visivyoonekana" kutoa joto la maji

Rais Zelenskiy amesema wa Ukraine wanaohitaji huduma za msingi endapo Urusi itaharibu vituo vya umeme na vifaa vingine msimu huu wa baridi, wanaweza kugeukia kile kinachoitwa vituo visivyoonekana.

Maelfu ya vituo hivyo vilivosambazwa nchi nzima vitatoa umeme, joto, maji, huduma za intanet, uunganishaji wa simu za viganjani na huduma za famasia bure na wakati wote.

Mashambulizi ya Urusi yamekatisha umeme kwa vipindi virefu kwa hadi watumiaji milioni 10 kwa wakati mmoja. Shirika la umeme la Ukraine lilisema jana kuwa uharibifu ni mkubwa mno.

Urusi imekuwa ikilenga vituo vya umeme nchini Ukraine na kusababisha mamilioni ya watu kukosa umeme kwa wakati mmoja na kwa muda mrefu.Picha: picture alliance / AA

''Endapo mashambulizi makubwa ya Urusi yatatokea tena na endapo tutakuwa na uelewa kwamba umeme hautarejeshwa katika saa chache, basi vituo visivyoonekana vitawashwa.

Mahitaji yote ya msingi yatatolewa - haya ni umeme, huduma za simu, intaneti, upashaji joto, maji, huduma ya kwanza na dawa," alisema Zelenskiy katika ujumbe wake wa vidio wa usiku.

Soma pia: Zelensky: Kipindi cha baridi Ulaya kitakuwa kigumu

Zelenskiy amesema tayari vituo zaidi ya 4,000 vimeundwa na vingine zaidi vinapangwa.

Nishati imegeuka lengo muhimu la operesheni ya Urusi nchini Ukraine, huku Zelenskiy na maafisa wengine wa Ukraine wakiwahimiza raia kuokoa umeme na kuhamisha matumizi kwenye saa zisizo za matumizi makubwa.

Urusi yalaani uvamizi wa jumba la watawa Kyiv

Kwa upande mwingine Urusi nayo imeilaani Ukraine kwa kufanya uvamizi kwenye nyumba ya zamani ya watawa wa Kiorthodox mjini Kyiv, ikiitaja kama nchi isiyomcha Mungu, wanyama na wakosefu wa maadili.

Soma pia: Urusi yaendelea kuishambulia Ukraine

Idara ya usalama ya Ukraine, SBU, pamoja na polisi walivamia nyumba hiyo ya miaka 1,000 mapema Jumanne, kama sehemu ya operesheni ya kukabiliana na vitendo vya uchochezi vya idara ya shughuli maalumu ya Urusi, ilisema SBU.

Mkuu wa SBU Ivan Bakanov na mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine Iryna Venediktova wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kyiv hivi karibuni.Picha: Photoshot/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova, amesema leo kuwa hakukuwa na sababu ya uvamizi huo, huku akiulinganisha utawala mjini Kyiv na Bacchus, mungu wa Kirumi wa divai, ambaye jina lake linahusishwa mara nyingi nchini Urusi na ghasia zisizo na maadili, machafuko na tafrija.

Kanisa la Orthodox la Urusi lilisema Jumanne kuwa msako huo ulikuwa kitendo cha kutishia. Kituo hicho ni hazina ya kitamaduni ya Ukraine na makao makuu ya tawi la Kanisa ya Kiorthodox la Ukraine linaloungwa mkono na Urusi ambalo liko chini ya Kanisa la Moscow.

Papa ahusisha masaibu ya wa Ukraine na mauaji ya kimbari ya Stalin

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis Jumatano aliunganisha mateso ya wa Ukraine sasa na "mauaji ya kimbari ya miaka ya 1930 yaliosababishwa na Stalin," wakati kiongozi huyo a Kisoviet alipolaumiwa kwa kuunda ukame uliosababishwa na mwanadamu nchini humo, unaoaminika kuuwa zaidi ya watu milioni 3.

Hatua ya Francis kuunganisha masaibu ya raia wa Ukraine leo na wale waliouawa kwa kunyimwa chakula miaka 90 iliyopita, na utayarifu wake kuyaita mauaji ya halaiki na kuyalaumu kikamilifu dhidi ya Josef Stalin,  imeashiria uchochezi mkubwa katika historia ya upapa dhidi ya Urusi.

Kufikia mwaka huu, ni mataifa 17 tu yaliotambua njaa hiyo, inayojulikana kama  Holodomor, kwa mujibu wa makumbusho ya Holodomor ya mjini Kyiv.

Soma pia: Pasaka yaadhimishwa Ukraine ikizidi kushambuliwa

Katika matamshi aliyoyatoa mwishoni mwa hadhira yake ya kila Jumatano, Francis alirudia wito wa sala kwa "mateso mabaya kwa watu wapendwa na waliouawa wa Ukraine." Amekumbushia kwamba Jumamosi itatimia miaka 90 tangu kuanza kwa njaa ambayo Ukraine inaiadhimisha kila Jumamosi ya nne ya mwezi Novemba kwa siku ya kumbukumbu.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW