1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAfrika

Al-Shabaab yautikisa tena mji mkuu wa Somalia

12 Januari 2022

Watu kadhaa wameuawa katika shambulizi la bomu katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, ambalo limedaiwa na kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab, lililosema katika taarifa fupi kwamba lilikuwa linawalenga maafisa wa kigeni.

Somalia | Anschlag in Mogadischu
Maafisa wa usalama wa Somalia wakilinda eneo la tukio la mlipuko katika wilaya ya Hamarweyne, katika mji mkuu wa Mogadishu, Januari 12, 2022.Picha: Feisal Omar/REUTERS

Shambulio hilo limetokea siku chache tu baada ya viongozi wa Somalia kukubaliana juu ya ratiba mpya ya uchaguzi uliocheleweshwa katika taifa hilo la pembe ya Afrika.

Serikali imesema katika taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, kwamba inalaani shambulio hilo la uoga la kujitoa muhanga, na kutaja idadi ya waliokufa kuwa wanne na majeruhi sita.

Taarifa hiyo ya serikali imesema vitendo kama hivyo vya kigaidi haviwezi kukwamisha amani na maendeleo yanayoshuhudiwa nchini humo, na kwamba laazima waungane katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Soma pia: Somalia yatumbukia kwenye mgogoro mpya

Awali afisa usalama wa serikali ya mji Mohamed Abdi aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kwamba watu wasiopungua sita walikuwa wameuawa, na kuongeza kuwa shambulio hilo lilisababisha pia uharibifu mkubwa kwenye eneo lilikotokea, huku akionya kwamba idadi ya vifo huenda ikawa kubwa zaidi kwa sababu idadi kubwa ya watu walikuwa eneo hilo.

Raia wakijaribu kuzima moto kwenye eneo la tukio la mlipuko katika wilaya ya Hamarweyne, mjini Mogadishu, Januari 12, 2022.Picha: Feisal Omar/REUTERS

Mashuhuda walisema msafara wa magari kadhaa ya ulinzi binafsi uliokuwa unawasindikiza wageni ulikuwa unapita karibu na eneo la tukio kusini mwa Mogadishu wakati mlipuko huo ulipotokea.

"Wakati tukiwa tunashughulika  kumsaidia mtu wa kwanza, tuliona mwanaume wa pili anaungua. Niliona maiti hapa, na nyingine pale. Moja ile pale na nyingine iko upande ule, akiwemo mwanajeshi," alisema shuhuda kwa jina la Abdiweli Mohamed Mohamud.

Soma pia: Somalia:Waziri mkuu amtuhumu Rais kuingilia uchunguzi kesi muhimu

Shuhuda mwingine Hassan Nur alisema shambulio hilo limekuwa kubwa sana kiasi kwamba liliharibu mengi ya majengo yalioko karibu na barabara na magari yaliokuwa yanapita karibu na eneo hilo.

Mzozo wa madaraka kati ya rais na waziri mkuu

Somalia imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu mwezi Februari mwaka jana, baada ya kushindwa kufikia makubaliano juu ya kuitishwa kwa uchaguzi.

Mkwano huo umesababisha mzozo mbaya wa madaraka kati ya rais Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmaji, na waziri mkuu wake Mohamed Hussein Roble.

Chini ya makubaliano yaliotangazwa Jumapili jioni baada ya mazugumzo kati ya Roble na viongozi wa majimbo, uchaguzi wa bunge ambao ulipaswa kukamilishwa mwaka uliyopita, hivi sasa umepangwa kukamilishwa Februari 25.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed, Farmajo (kushoto) na waziri mkuu Mohamed Hussein Roble (kulia), wakiwa katika hafla ya ufungaji baada ya kufikia muafaka kuhusu uchaguzi mpya wa Somalia, Mei 27, 2021.Picha: Abdirahman Yusuf/AFP/Getty Images

Makubaliano hayo yalionekana kutulizwa mzozo kati ya Roble na Farmajo, ambaye alisema katika taarifa Jumatatu jioni kwamba anapongeza matokeo chanya kuhusu ratiba ya uchaguzi.

Mzozo huo ulizusha wasiwasi miongoni mwa jumuiya ya kimataifa, inayohofia kwamba unatishia utulivu wa taifa hilo tete linalokabiliana bado na uasi wa vurugu wa kundi la Al-Shabaab.

Soma pia:Viongozi kuharakisha mchakato wa uchaguzi Somalia 

Kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limekuwa likiendesha kampeni kali ya mashambulizi dhidi ya serikali kuu dhaifu tangu 2007, lakini walifurushwa kutoka mji wa Mogadishu mnamo 2011, kufuatia mashambulizi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika.

Hata hivyo wapiganaji hao wanabakisha udhibiti wa maeneo makubwa ya viji vya Somalia, ambako wanatokea mara kwa mara na kufanya mashambulizi ya kutisha katika mji mkuu na kwingineko dhidi ya maeneo ya kiraia, jeshi na serikali.

Chanzo: Mashirika