1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la droni latikisa Crimea, ghala la silaha lalipuka

Angela Mdungu
22 Julai 2023

Gavana wa Crimea anayeungwa mkono na Urusi amesema, shambulio la droni lililoelekezwa katika ghala la mabomu kwenye rasi hiyo lilizilazimu mamlaka zimuondoe kila mtu aliye ndani ya umbali wa kilometa tano.

Daraja la Crimea
Daraja la CrimeaPicha: Alexander Nemenov/AFP

Shambulio hilo limesababisha pia kusitishwa kwa usafiri wa barabara katika daraja linaloiunganisha Crimea na Urusi. Hata hivyo baadaye, ukurasa rasmi wa mamlaka za Crimea ulitangaza kuwa shughuli za usafiri zimeanza tena baada ya kusitishwa kwa muda mapema Jumamosi.

Gavana huyo, Sergei Aksyonov kupitia ukurasa wake wa Twitter liandika kuwa kulitokea mlipuko kwenye ghala hilo huko Krasnohvardiiske katikati mwa Crimea. Hakuna majeruhi wala uharibifu ulioripotiwa kutokana na shambulio hilo.

Video iliyotolewa na shirika la habari la Urusi ilionesha wingu nene la moshi wa kijivu katika eneo la tukio. Aksyonov ameinyooshea kidole cha lawama Ukraine kwa kuhusika na shambulio hilo. Kyiv haikupatikana kwa haraka kutoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.

Soma zaidi: Shambulizi la Ukraine laharibu daraja la Crimea: Urusi

Urusi iliidhibiti Crimea na kuiweka chini ya utawala wake kutoka kwa Ukraine mwaka 2014 kabla ya kuivamia nchi hiyo miaka nane baadaye.

Muonekano wa daraja la Crimea baada ya shambulio la Julai 17,2013Picha: Сrimea24tv via REUTERS

Huduma za usafiri wa barabara zimesimamishwa kwenye daraja la Crimea, siku tano baada ya kutokea kwa mlipuko uliowauwa watu wawili na kufanya uharibifu sehemu ya barabara. Shambulio hilo linatajwa kuwa ni la pili kwa ukubwa kuelekezwa katika daraja hilo tangu vita vilipoanza.

Barabara ya kilometa 19 na daraja hilo ni kiungo muhimu kwa upitishaji wa vifaa vya majeshi ya Urusi na linatumika pia pakubwa na watalii wa Urusi wanaofurika kuelekea kwenye rasi ya Crimea wakati wa majira ya joto.

Urusi yailaumu Ukraine, Kyiv bado haijakiri kuhusika

Urusi inaituhumu Ukraine kwa mashambulizi kwenye daraja hilo. Maafisa wa Kyiv wamepongeza  mashambulizi hayo bila kukiri kuwa wamehusika ama la. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Ijumaa kuwa daraja hilo ni eneo muhimu wanalolilenga kwa kuwa ni njia inayotumiwa kusambaza vifaa vya kijeshi kwa Urusi.

Mashambulizi katika rasi hiyo ya Bahari Nyeusi yamekuwa yakishika kasi katika wiki za hivi karibuni, huku Kyiv ikijibu mashambulizi ya kutaka kuirejesha Crimea mikononi mwake

Itakumbukwa kuwa, barabara zilifungwa kwenye daraja hilo Jumatatu,  baada ya kutokea kwa shambulizi lililosababisha vifo vya watu wawili. Daraja hilo ndiyo kwanza lilikuwa limeanza tena kufanya kazi baada ya kuharibiwa na mlipuko wa bomu Oktoba mwaka uliopita.

Wakati huohuo, Gavana wa Belgorod Vyacheslav Gladkov amesema Ukraine ilitumia mabomu ya mtawanyiko kushambulia eneo la mpaka la Belgorod. Amesema, Kyiv ilichambulia kijiji cha Zhuravlyovka kwa roketi zilizorusha mabomu hayo katika tukio ambalo hakuna majeruhi wala uharibifu ulioripotiwa.

Mkaazi akishuhudia sehemu ya uharibifu uliotokana na mashambulizi BelgorodPicha: AFP

Hivi karibuni Marekani iliipatia Ukraine mabomu ya mtawanyiko ili ijilinde na mashambulizi ya Urusi licha ya ukosoaji mkali kimataifa. Zaidi ya mataifa 100 ikiwemo Ujerumani, yalitia saini makubaliano ya kuharamisha matumizi ya silaha za aina hiyo.

Mashambulizi yaendelea kurindima pia upande wa Ukraine

Katika hatua nyingine, mashambulizi yaliyofanyika usiku kucha katika maeneo 11 ya Ukraine yamesababisha vifo vya karibu raia 8. Mamlaka za Kyivv zinasema watu wengine watatu wamelazwa hospitali baada ya kujeruhiwa kutokana na matukio hayo.

Mwendesha mashitaka wa kanda huko mashariki mwa Donesk amesema kati ya watu wanne waliouwawa  baada ya Urusi kufanya mashambulizi huko Niu-York kusini mwa Bakhmut, wawili kati yao walikuwa ni wanandoa. Mji wa Bakhmut umekuwa uwanja wa mapambano katika vita vya Urusi na Ukraine tangu vilipoanza mwezi Mei.

Wanajeshi wa Ukraine katika uwanja wa mapambano DoneskPicha: Diego Herrera Carcedo/AA/picture alliance

Mapema Jumamosi wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine ilisema kuwa raia wengine wawili waliuwawa baada ya vikosi vya Urusi kushambulia mji wa Kostiantynivka, na raia mwingine mmoja amejeruhiwa katika tukio hilo hilo. 

Mamlaka za jeshi ziliripoti kuwa watu wengine wawili waliuwawa pia kwenye mkoa wa Donetsk karibu na mji ulio kaskazini wa Chernihiv, kilomita 100 kutoka mpakani na Urusi. Ni baada ya Urusi kurusha kombora lililosaabisha uharibifu kwenye kituo cha utamaduni wa ndani na kuharibu makazi ya watu. Hata hivyo muda lilipotokea shambulio hilo haukutajwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW