Shambulio la sumu Syria; 40 wauwawa
8 Aprili 2018Taarifa ya pamoja ya shirika la kutoa msaada wa matibabu la chama cha madaktari wa Syria na Marekani (SAMS) na huduma za ulinzi wa raia mashirika yanayofanya shughuli zake katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi, zimesema watu 49 wamefariki katika shambulio hilo jioni ya Jumamosi. Wengine wanasema idadi ni watu 150 ama zaidi.
Tangu kuanza kwa mzozo wa Syria mwaka 2011, taifa hilo lililomo katika vita, hususan utawala wa rais bashar al-Assad, umeshutumiwa katika nyakati kadhaa kwa kutumia silaha za sumu.
Marekani imeionyooshea kidole leo Jumapili Urusi kuhusiana na madai ya shambulio la sumu mjini Douma, ngome ya mwisho ya waasi katika eneo la Ghouta Mashariki, baada ya zaidi ya watu 80 kuuwawa katika mashambulizi ya mwishoni mwa juma.
Marekani imesema iwapo itathibitishwa Urusi itawajibika kutokana na "uungaji mkono usioyumba" kwa utawala huo. Urusi inakana kwamba utawala wa Syria ulitumia silaha za sumu.
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis leo ameshutumu shambulio la gesi ya sumu lililoripotiwa nchini Syria kuwa ni matumizi ambayo yanayokwenda kabisa kinyume na sheria ya "vifaa vya maangamizi".
White Helmets, kundi ambalo huchukua hatua wakiwa wa kwanza kutoa misaada katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi nchini Syria, linadai kwamba majeshi ya serikali yalitumia "gesi ya sumu ya klorini" katika mashambulizi, dai ambalo vyombo vya habari vya dola vinakana.
Shirika linalopambana dhidi ya matumizi ya silaha za sumu
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria linaripoti kwamba darzeni kadhaa za watu waliathirika kutokana na matatizo ya kushindwa kupumua kufuiatia shambulio la majeshi ya serikali, lakini halikutambua sababu ya hali hiyo.
Shirika linalopambana dhidi ya matumiziya silaha za sumu na kutaka kupigwa marufuku silaha hizo (OPCW) limesema limechunguza mashambulio 70 ya gesi nchini Syria tangu mwaka 2014, kutoka matukio 370 yaliyoripotiwa.
Mwezi Agosti 2013 majeshi ya serikali yalifanya mashambulio Ghouta mashariki na Moadamiyet al-Sham, maeneo yanayoshikiliwa na waasi nje ya mji wa Damascus.
Upinzani unaushutumu utawala wa nchi hiyo kwa shambulio kubwa la gesi ya sumu. Serikali, ambayo imekiri mwaka 2012 kwamba ina silaha za sumu, inakana madai hayo.
Ripoti ya kijasusi ya Marekani inasema kwa "kujiamini kabisa" kwamba serikali ya Syria ilifanya mashambulio hayo. Inasema watu 1,429 wameuwawa, ikiwa ni pamoja na watoto 426. Licha ya kusisitiza kwamba matumizi ya silaha za sumu ni kuvuka msitari mwekundu , rais Barack Obama hakuweza kushambulia syria kama jibu la matumizi hayo ya gesi ya sumu.
Marekani badala yake iliamua kutumia diplomasia na kuingia katika makubaliano na Urusi kwamba inapaswa kuangalia kwamba hazina ya silaha za sumu za utawala huo zinaharibiwa.
Katikati ya mwezi Septemba ripoti ya Umoja wa mataifa ilisema kuna ushahidi wa wazi kwamba gesi ya sarin ilitumika.
Wakati huo huo vyombo vya habari vya serikali nchini Syria vinaripoti kwamba waasi katika eneo la Ghouta mashariki wameomba kuanza tena mazungumzo ili kuzuwia mashambulizi ya majeshi ya serikali katika mji ambao ndio ngome yao ya mwisho katika kitongoji cha Ghouta karibu na mji mkuu Damascus.
Televisheni inayohusiana na serikali ya Al-Ikhbariya imeripoti kwamba serikali imetaka kundi la wanamgambo wa Jeshi la Waislamu wawaachie huru mateka na kusitisha mashambulio yao dhidi ya mji mkuu Damascus kama sharti la kuanza mazungumzo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Oummilkheir Hamidou