Shambulio la Urusi laua watu sita Ukraine
2 Novemba 2025
Watu sita wakiwemo watoto wawili wameuwawa kufuatia shambulio la droni katika mkoa wa Kusini Magharibimwa Ukraine wa Odesa. Taarifa hizo zimetolewa leo Jumapili na mamlaka nchini Ukraine ambapo imeelezwa kwamba droni za Urusi zilishambulia eneo la kuegesha magari kwenye eneo hilo mapema leo Jumapili na kuuwa watu sita na wengine watatu walijeruhiwa.
Ripoti pia zinasema kwamba Urusi imeendelea kushambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine. Maelfu ya wakaazi walikaa bila umeme baada ya Urusi kushambulia mkoa wa Zaporizhzhia usiku wa kuamkia leo Jumapili kwa droni na makombora.
Gavana wa eneo hilo Ivan Fedorov amesema takriban watu 60,000 walikosa umeme na watu wawili walijeruhiwa kufuatia mashambulio hayo ambayo ndiyo ya karibuni zaidi kufanywa na Urusi katika kampeni yake inayolenga miundombinu ya nishati yaUkraine wakati majira ya baridi kali yakikaribia.