Shambulizi la bomu laua watu 30 Nigeria
9 Mei 2014Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Punch la Nigeria, bomu hilo lililupuka jana jioni nje kidogo ya kijiji cha Gamboru Ngala ambacho kwa wiki hii tu kimeshuhudia zaidi ya watu 200 wakiuwawa huku wasichana 11 wakitekwa na kundi hilo la Boko Haram.
"Ninaamini kuna watu wengine bado wamefukiwa katika vifusi" mkazi mmoja wa kijiji hicho aliliambia gazeti hilo. Mlipuko huo wa bomu umetokea wakati ambapo mataifa kadhaa yamejitokeza kuisaidia Nigeria kuwatafuta wanafunzi wasichana zaidi ya mia mbili waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram wiki tatu zilizopita.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amekiri kuongea na baadhi ya mataifa yanayotaka kusaidia kuwatafuta wanafunzi hao. Ikulu ya Marekani imesema maafisa wa kijeshi wa nchi hiyo watawasili Nigeria siku tatu zijazo, pamoja na wataalamu wa mazungumzo na wateka nyara na wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba kutoka shirika la upelelezi la nchi hiyo FBI.
Wakatii huo huo kampeni za kushinikiza kundi hilo la Boko Haram kuwaachia wanafunzi hao, zimeendelea duniani kote kwa watu maarufu kuzidi kujitokeza, mke wa rais wa Marekani Michelle Obama amejiunga na mtandao wakijamii unaopinga kitendo cha kutekwa nyara wasichana hao.
"Sala zetu tunazielekeza kwa wasichana wa Nigeria waliotekwa pamoja na familia zao, ni muda sasa wa kuwarudisha watoto wetu" aliandika Michelle Obama chini ya picha aliyotuma katika mtandao huo wa kijamii ambayo ilitumwa pia na zaidi ya watu 48,000.
Ofisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulika na masuala ya haki za binadamu imetoa onyo kwa kundi la Boko Haram kwamba watahukumiwa kwa kutenda uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Polisi wa Nigeria wameahidi zaidi ya dola laki tatu kwa yeyote atakayetaja mahali walipo wanafunzi hao ambao walitekwa April 14 wakiwa katika mabweni ya shule yao iliyopo Chobok karibu na mjii mkuu wa jimbo la Borno.
Mwandishi: Anuary Mkama
Mhariri: Yusuf Saumu