Shambulizi la droni laua watu 32 Darfur Kaskazini
10 Aprili 2026
Shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye mji wa Kutum unaodhibitiwa na wanajeshi katika jimbo la Darfur Kaskazini mwa Sudan limewaua raia wasiopungua 32, wakiwemo wanawake na watoto.
Hayo ni kwa mujibu wa chanzo cha matibabu na wakazi watatu waliozungmza na shirika la habari la AFP jana Alhamisi.
Kamati ya Upinzani ya El-Fasher, kundi linalounga mkono demokrasia, lilisema shambulio hilo lilipiga kitongoji cha Al-Salama na kulaumu jeshi kwa shambulio hilo.
Chanzo cha matibabu hapo awali kiliiambia AFP kwamba miili 12 ililetwa hospitalini huko Kutum, nusu yao ikiwa ni ya watoto, wakiwemo wanafunzi watatu wa kike wa shule ya upili.
Wengine kumi na sita walijeruhiwa, wakiwemo wanawake na watoto, na wanapokea matibabu, chanzo hicho kiliongeza, kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama.
Jeshi bado halijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo. RSF, wakati huo huo, ilililaani katika taarifa na kuweka idadi ya vifo kuwa si chini ya 56, wakiwemo watoto 17.