1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Shambulio lasababisha raia 40,000 kukosa umeme Ukraine

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2024

Ukraine imesema kwamba shambulizi la mkururo wa droni za Urusi limeharibu miundombinu ya nishati katikati mwa nchi hiyo na kusababisha maelfu ya watu kukosa umeme.

Jumba la maakazi mjini Kyiv lililoshambuliwa na Urusi
Jumba la maakazi mjini Kyiv lililoshambuliwa na UrusiPicha: Danylo Pavlov/REUTERS

Jeshi la anga la Ukraine limedai kuwa Moscow imerusha ndege zipatazo 24 za droni zilizobuniwa Iran na kuharibu miundombinu ya shirika la ugavi wa nishati la taifa kwenye mkoa wa Dnipropetrovsk.

Jeshi hilo pia limesema mfumo wake wa ulinzi umefanikiwa kuzidungua droni 11.

Mkuu wa mkoa huo Sergiy Lysak ameandika kupitia mitandao ya kijamii kwamba wakaazi takribani 40,000 wamekosa umeme pamoja na migodi miwili.

Shambulio hilo la usiku wa jana linarejesha kumbukumbu ya mashambulizi ya mara kwa mara yaliyofanywa na Urusi wakati wa msimu uliopita wa baridi, ambayo yalisababisha mamilioni ya Waukraine kukosa umeme au maji kwa muda mrefu.