1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Israel laua wapiganaji wa Hezbollah

6 Agosti 2024

Wapiganaji watano wa Hezbollah wameuawa katika shambulizi la anga la Israel lililokilenga kijiji kimoja kusini mwa Lebanon, huku kundi hilo likianzisha mashambulizi ya droni na roketi kaskazini mwa Israel.

Jeshi la Israeli lashambulia kijiji cha kusini mwa Lebanon
Jeshi la Israeli lashambulia kijiji cha kusini mwa LebanonPicha: Ramiz Dallah/Anadolu/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na wizara ya afya ya Lebanon imeeleza kuwa mashambulizi ya Israel yamefanyika Jumanne na shughuli ya kuondoa kifusi kuwatafuta waathirika zaidi zinaendelea. Duru za usalama za Lebanon zimeeleza kuwa katika tukio jengine, mtoto mmoja amejeruhiwa kwa shambulizi la kombora la Israel kwenye eneo la Al-Wazzani, kusini mwa Lebanon.

Jeshi la Israel limesema kikosi chake cha anga kimeshambulia eneo la kijeshi la Hezbollah katika mji wa Nabatiyeh, ambalo lilikuwa linatumika kutekeleza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel.

Soma zaidi: Hofu yaongezeka kuhusu kutanuka kwa mzozo Mashariki ya Kati

Hayo yanajiri wakati ambapo kundi la Hezbollah Jumanne limeanzisha mfululizo wa mashambulizi ya droni na roketi kuelekea kaskazini mwa Israel. Kulingana na kundi hilo, shambulizi la droni limeanzishwa kwenye maeneo mawili ya kijeshi karibu na Acre, kaskazini mwa Israel ikiwemo jengo linalotumiwa na wanajeshi wa Israel huko Avivim, na pia limeshambulia gari la jeshi la Israel kwenye eneo jingine.

Nyumba zilizoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel huko LebanonPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Jeshi la Israel limesema idadi kadhaa ya droni ziligunduliwa zikirushwa kutoa Lebanon na moja ilizuiwa. Maafisa wa afya wa Israel wamesema watu saba wamepelekwa hospitali kusini mwa mji wa Nahariya, huku mmoja akiwa mahututi. Israel imesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa raia kadhaa walijeruhiwa na droni iliyozuiwa ambayo ilishindwa kushambulia eneo husika na kuangukia ardhini, na kwamba tukio hilo bado linachunguzwa.

Juhudi zinaendelea kuhakikisha mzozo hauongezeki

Kundi la Hezbollah limesema mashambulizi hayo ni katika kujibu shambulizi la anga lililofanywa na jeshi la Israel katika kijiji cha Ebba siku ya Jumatatu, ambalo lilimlenga kamanda wa kikosi maalum cha Hezbollah cha Radwan.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Abdallah Bou Habib amesema kuwa nchi yake inafanya kazi kuhakikisha kuwa ulipizaji kisasi kwa Israel hauchochei vita kamili. Matamshi hayo ameyatoa Jumanne katika mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Abdallah Bou HabibPicha: Kira Hofmann/photothek/picture alliance

''Hii ni kwa sababu vita havitoinufaisha nchi yoyote inayohusika, ikiwemo Israel. Ni wale tu wanaotaka kuchochea migogoro ndiyo watanufaika na hali hiyo. Sisi, kama maafisa, hatutaki vita vyovyote. Hivyo, iwapo ulipizaji kisasi utakuwa lazima, unapaswa kutokuwa vita kamili ambayo inaweza kuenea na kuwa mzozo mkubwa zaidi,'' alifafanua Habib.

Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty amezungumzia umuhimu wa uratibu wa kimataifa kati ya Misri na Marekani. Mwanadiplomasia huyo wa Misri anasema kuna makubaliano ya wazi baina ya nchi kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kusitisha kuenea kwa mzozo na kushughulikia matokeo yoyote ya hatari kwa usalama na utulivu katika kanda.

Wasiwasi unaongezeka kwamba Mashariki ya Kati huenda ikaingia kwenye vita kamili kutokana na Hezbollah kuapa kwamba italipiza kisasi mauaji ya kamanda wa Hezbollah Fuad Shukr, na Iran kujibu mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Palestina la Hamas Ismail Haniyeh, aliyeuawa wiki iliyopita mjini Tehran.

(AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW