Shambulizi la kemikali Syria"uongo" mtupu-Assad
13 Aprili 2017Hayo yanajiri huku rais Bashar al Assad akidai serikali yake ilisingiziwa kwa asilimia 100 kuwa ilihusika katika shambulizi la sumu ya gesi mkoa wa Idlib lilosababisha maafa ya zaidi ya watu 80. Katika mahojiano ya kipekee na shirika la habari la AFP katika ikulu ya rais mjini Damascus nchini Syria ,al-Assad amesema kimaadili serikali yake haiwezi kufanya kamwe shambulizi hatari kama hilo kwasababu halikubaliki. Kiongozi huyo ambae anapambana katika vita vinavyonuia kumwondoa madarakani tangu taifa lake kutumbukia katika mapigano miaka sita iliyopita,amesema hatishiki na shambulizi liloamriwa na rais wa Marekani Donald Trump,na kukiri kuwa anatazamia kufanyika mashambulizi zaidi. Rais Assad amesisitiza kuwa vikosi vyake viliacha kutumia silaha zote za sumu miaka mingi iliyopita na haviwezi kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku. Mahojiano hayo na shirika la habari la AFP yalikuwa ya kwanza tangu kutokea shambulizi la silaha za sumu tarehe 4 mwezi huu lilosababisha mauji ya watu chungunzima wakiwemo watoto 31 katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Khan Sheikhun. Rais huyo wa Syria amesema ushahidi kuhusu shambulizi hilo ulitolewa tu na kundi la wapiganaji wa Al-Qaeda akimaanisha lilokuwa kundi la wapiganaji ,ambalo ni miongoni mwa makundi mengine yanayosimamia mkoa huo wa Idlib. Picha za baada ya shambulizi zilizowaonyesha waathiriwa baadhi yao watoto waliokuwa wakitokwa na povu mdomoni ziliushtua ulimwengu mzima. Hata hivyo Assad anashikilia kusema kwamba ni vigumu kubaini iwapo shambulizi hilo lilitokea kwa kuwa hakuna anayeweza kuithibitisha video hiyo kutokana na kuzangaa video za kutengenezwa.
Marekani yalaumiwa kuwaua raia
Taarifa nyingine ni kuwa serikali ya Syria imesema mashambulizi yanayofanywa na Marekani nchini humo yameendelea kuwaua mamia ya raia.Katika tukio la hivi karibuni vikosi hivyo vya Marekani vinadaiwa kuushambulia mkoa wa Deir al Zor na kuwaua mamia ya watu wakiwemo raia. Hata hivyo msemaji wa kikosi cha Marekani John Dorrian ameyakanusha madai hayo na kusema si ya kweli. Hata hivyo Marekani imekiri kuwa iliwaua kimakosa wapiganaji 18 wa kikosi cha democrasi nchini Syria-SDF kufuatia shambulizi la angani. Kikosi hicho kinachowajumuisha Wakurdi na Waarabu kinaungwa mkono na Marekani. Hata hivyo SDF kimesema kitaendelea na harakati zake za kukabiliana na wapiganaji wa IS licha tukio hilo. Vikosi vya marekani hata hivyo vimesema vinatathmini kilichosababisha makosa hayo ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Mwandishi:Jane Nyingi AFP/AP
Mhariri:Yusuf Saumu