1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la kigaidi lawauwa watu 56 Niger

3 Januari 2021

Watu wenye silaha wamewauwa raia 56 na kujeruhi wengine 20 katika shambulizi baya kabisa nchini Niger lililotokea siku ya Jumamosi.

Niger Symbolbild Terror
Picha: Boureima Hama/AFP

Taarifa iliyotolewa na waziri wa mambo ya ndani wa Niger Alkache Alhada imesema shambulizi hilo limetokea kwenye vijiji vya Tchomb-Bangou na Zaroumdareye vilivyo jirani na mpaka na kati ya nchi hiyo na Mali.

Afisa mwingine wa serikali ambaye amezungumza na shirika la habari la AFP amesema "shambulizi lilitokea majira ya [Jumamosi] mchana na kumetokea vifo", bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi kuhusu shambulizi lenyewe.

Afisa mwingine wa serikali ya eneo hilo naye amenukuliwa akisema "watu wengi wameuwawa" kwenye shambulizi katika kijiji cha Tchomo-Bangou kilichopo karibu na mpaka wa Niger na Mali lakini naye pia hakufafanua zaidi kile kilichotokea.

Majonzi wakati wa matokeo ya uchaguzi wa rais

Shambulizi hili limetokea siku ambayo maafisa wa uchaguzi wametangazamatokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Nigerambayo yanaonesha mgombea wa chama tawala na waziri wa zamani Mohamed Bazoum anaongoza lakini kwa asilimia chache inayolazimisha kufanyika duru ya pili baadaye mwezi unaokuja.

Mgombea wa chama tawala nchini Niger, Mohamed BazoumPicha: Issouf SANOGO/AFP

Bazoum amepata asilimia 39.6 wakati mgombea wa upinzani Mahamane Ousmane amejikingia asilimia16.

Ousmane alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Niger hadi alipondolewa katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1996.

Bazoum ni mshirika wa karibu wa rais Mahammadou Issoufou, ambaye anamaliza muda wake baada ya kutawala mihula miwili ya miaka mitano.

Niger na uthabiti dhaifu katika kanda ya Sahel

Niger, moja ya taifa linaloandamwa na hali dhaifu ya kiusalama kwenye kanda ya Sahel, magharibi mwa Afrika, imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya makundi ya itikadi kali yanayowania udhibiti wa kanda hiyo.

Picha: AFP/S. Ag Anara

 

Makundi hayo, mengi yenye mafungamano na kundi la itikadi kali la Al-Qaeda na jingine linalojiita Dola la Kiislamu, IS, yanaitikisa kanda ya Sahel yenye mataifa matano ya Niger, Burkina Faso, Chad, Mali na Mauritania.

Kwa muda sasa imekuwa vigumu kwa mamlaka za mataifa hayo kusimamia uthabiti wa kanda hiyo katika jangwa la Sahara.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, Minusma, pamoja na Ufaransa na Marekani zimekuwa zikitoa msaada wa kupambana na makundi ya itikadi kali kwenye kanda hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW