1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Orlando ni la kutisha na hatari

13 Juni 2016

Magaidi siku zote wana angalau malengo mawili pindi wanapofanya mashambulizi. Wanakusudia kuwaua watu wanaowalenga, na pia kuharibu kabisa maeneo ya wazi ya kijamii. Haya ni maoni ya mwandishi wa DW Washington, Ines Pohl

Maafisa wa polisi wa Orlando
Maafisa wa polisi wa OrlandoPicha: Reuters/K. Kolczynski

Shambulizi katika klabu ya usiku huko Orlando, Marekani lililowaua kiasi ya watu 50, ni janga ambalo sio tu la kutisha, bali pia la hatari. Katika mwaka huu wa uchaguzi, mshambuliaji huyo wa Orlando huenda akafanikiwa kwa malengo hayo.

Shambulizi hilo la Orlando limetokea wakati ambapo Marekani imejikuta iko katikati mwa mtihani muhimu. Marekani ambayo ndiyo kwanza iko mwanzoni mwa mapambano kuhusu swali la nani ataingia katika Ikulu ya White House kama rais ajaye wa nchi hiyo. Shambulizi hilo limetokea wakati ambapo uchaguzi wa urais umeanza kupamba moto.

Muda mfupi baada ya shambulizi kutokea, wafuasi wa Donald Trump, wameonyesha jinsi gani wangeweza kumaliza kitendo hiki cha ugaidi. Wameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter wakimpongeza Trump kuhusu msimamo wake wa kupambana na Uislamu katika mtazamo dhahiri wa dini ya mshambuliaji.

Msimamo wa Hillary kutumiwa dhidi yake

Hatua ya Hillary Clinton kuwa karibu na kuonyesha mshikamano na Waislamu, ni suala ambalo watalitumia dhidi yake. Watautumia mwanya wa hofu ya watu kumuweka kileleni mgombea wao. Kwa mwaka huu hasa, Wamarekani wengi wanaonekana kukabiliwa na vuguvugu la aina hii la kisiasa.

Ines PohlPicha: DW/I. Pohl

Wakati Donald Trump aliposema anataka kuifanya Marekani kuwa nzuri tena, akilini mwake alikuwa na nchi ambayo atakuwa kama mwenyeji mbabe. Hatua hiyo ni kile kilicho nyuma ya mpango wake wa kupiga marufuku kwa muda Waislamu kuingia Marekani, wasiwasi kuhusu jaji mwenye asili ya Mexico au udhalilishaji dhidi ya wanawake.

Mashambulizi ya kigaidi yanaweka changamoto kubwa katika kila jamii ya wazi. Mashambulizi hayo yanawalazimisha kujiuliza maswali magumu kuhusu thamani ya uhuru wao. Ni wajibu mgumu kwa wanasiasa na watu kukabiliana kwa utulivu na kuwa na mtazamo wa pamoja kuhusu hisia ya chuki na kisasi ambavyo vinaonyeshwa kupitia ugaidi. Rais Francois Hollande wa Ufaransa, alifanikiwa kwa kufanya hivyo, baada ya mashambulizi ya Paris. Aliwaongoza vyema watu wake.

Lakini kampeni za uchaguzi zinaanza nchini Marekani, mambo ambayo dunia haijawahi kamwe kushuhudia. Je Marekani ya 2016 itafanikiwa kuepukana na mtego uliowekwa na magaidi, katika kile ambacho kinaonekana kukosekana kwa uhuru kinachotarajiwa kufanywa na Waislamu wenye itikadi kali? Au itaweza kuitetea ndoto ya Marekani, ambayo kwa kiasi kikubwa imejengwa katika jamii ya wazi ya wahamiaji? Uwezekano ni kwamba ghadhabu ya kipofu itashinda.

Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Grace Patricia Kabogo/DW http://bit.ly/25T5nFC
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi