1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Shambulizi la Pakistan lauwa zaidi ya watu 400 Afghanistan

17 Machi 2026

Zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine 250 kujeruhiwa katika shambulio la anga lililofanywa na Pakistan dhidi ya kituo cha matibabu cha waraibu wa dawa za kulevya mjini Kabul nchini Afghanistan.

Pakistan Kohat 2026 | shambulizi la Pakistan nchini Afghanistan
Ibada ya mazishi kwa waathiriwa wa shambulizi la Paksitan mkoani Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan mnamo Februari 27, 2026Picha: Basit Shah/AFP

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Afganistan Abdul Mateen Qanie, amethibitisha kuuawa kwa watu hao 408 pamoja na kuwepo kwa majeruhi 265. Mamlaka ya nchi hiyo imesema waliokufa na waliojeruhiwa walipelekwa hospitali karibu na Kabul .

Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya afya nchini humo Sharafat Zaman, amewaambia waandishi wa habari kwamba idadi hiyo sio ya mwisho kwasababu operesheni ya uokoaji bado inaendelea .

Kwa upande wake, naibu msemaji wa kundi hilo la Taliban Hamdullah Fitrat, amesema shambulizi hilo lilitokea usiku wa jana Jumatatu na kulenga hospitali ya Omid inayoendeshwa na serikali na ambayo amesema ina idadi ya vitanda 2,000.

Sehemu kubwa ya hospitali ya Omid yaharibiwa

Kwenye chapisho katika mtandao wa X, Fitrat amesema sehemu kubwa ya hospitali hiyo imeharibiwa na kuna hofu ya kuweko kwa idadi kubwa zaidi ya waliokufa.

Ameongeza kusema timu za uokoaji ziko katika eneo hilo kukabiliana na moto wa shambulizi hilo pamoja na kutafuta manusura.

Afisa mmoja wa uokoaji Sayed Mehrab Shah ametoa maelezo kuhusu hali ilivyokuwa:

"Mlipuko ulipotokea, tuliarifiwa kupitia kituo cha ambulansi cha Kabul kwamba mlipuko mkubwa umetokea katika eneo lenye vitanda 1,000 la kituo hicho cha matibabu ya waraibu wa dawa za kulevya. Tulifika hapa na wafanyakazi wetu wote, na majeruhi walikuwa wakiletwa kwetu kutoka pande zote."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Lin Jian katika mkutano na waandishi wa habari mnamo Februari 9, 2026 mjini BeijingPicha: Kyodo/picture alliance

Hata hivyo, Reuters haikuweza kuthibitisha idadi ya waathiriwa. Katika mzozo huo, pande zote mbili zimedai kuwa zimesababisha uharibifu mkubwa kwa upande mwingine lakini madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru.

Huku hayo yakijiri, waziri wa habari wa Pakistan Attaullah Tarar, amesema kuwa mlipuko wa pili uliotokea baada ya shambulizi hilo, unaonyesha uwepo wa hifadhi kubwa ya risasi.

China yatoa wito wa utulivu kati ya Afghanistan na Pakistan

China imesema leo kuwa inatumai ⁠Afghanistan na Pakistan zitadumisha utulivu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa nchi hiyo Lin Jian, amesema nchi yake itaendelea kutekeleza jukumu muhimu kupitia njia zake ili kupunguza mivutano na kuboresha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mara nyingine tena, China imetoa wito wa kuhakikishwa kwa usalama wa wafanyakazi wake, miradi na taasisi zake katika kanda hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW