1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Urusi lauwa watu watano Ukraine

30 Agosti 2022

Watu wapatao watano wameuawa Ukraine baada ya kombora la Urusi kuushambulia mji wa Kharkiv, wakati ambapo majeshi ya Ukraine yakiendeleza operesheni za kulikomboa eneo la kusini linalodhibitiwa na Urusi la Kherson.

Ukraine-Krieg | Kämpfe in der Region Cherson
Picha: SERGEY BOBOK/AFP/Getty Images

Meya wa mji wa Kharkiv, Igor Terekhov amesema kwamba watu hao wameuawa katika shambulizi la kombora lililofanywa Jumanne asubuhi ambapo watu wengine saba wamejeruhiwa. Akizungumza kupitia mtandao wa Telegram, Terekhov amesema wanajeshi wavamizi wa Urusi wameshambulia katikati ya mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, ulioko kilomita 50 kutoka kwenye mpaka wa Urusi.

Naye mkuu wa tawala za kijeshi wa jimbo la Kharkiv, Oleg Synegubov amewataka raia kubakia ndani ya nyumba zao ili kuepuka maafa zaidi. Maafisa wamseama mji wa Kharkiv umekuwa ukishambuliwa vibaya waakti wote wa vita, huku mamia ya watu wakiuawa.

Wawili wauawa Mykolaiv

Hata hivyo, vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kuzuia juhudi za vikosi vya Urusi kutaka kuuchukua mji huo ambao ulikuwa na wakaazi wapatao milioni 1.4 kabla ya vita.

Aidha, maafisa wa mji wa Mykolaiv na watu walioshuhudia wamesema makombora ya Urusi yameshambulia maeneo ya makaazi kwenye mji huo na kuwaua raia wawili na kuziharibu nyumba kadhaa.

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Gleb Garanich/REUTERS

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyataka majeshi ya Urusi kukimbia kwenye mji wa Kherson baada ya vikosi vyake kuanzisha mashambulizi ya kuukomboa mji huo wa kusini, akisema majeshi yake yanalinyakua tena eneo lao. Majeshi ya Ukraine yameendeleza operesheni iliyoanza Jumatatu ya kulikomboa tena eneo hilo la kusini linalodhibitiwa na Urusi.

''Nina uhakika wote mnaelewa kinachoendelea na kile tunachokipigania na tunachokitaka. Wanajeshi wetu hawahitaji kujitangaza. Ukraine inayarejesha maeneo yake ya Kharkiv, Lugansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson, Crimea na kwa hakika maeneo yetu katika Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov,'' alisisitiza Zelensky.

Urusi nayo imeishutumu Ukraine kwa kuanzisha mashambulizi mapya katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia. Shirika la habari la Urusi la TASS limewanukuu maafisa waliowekwa na Urusi katika mji wa Enerhodar wakisema kuwa makombora mawili yameripuka karibu na jengo la kuhifadhia mafuta katika kinu hicho.

Ujumbe wa shirika la IAEA unaoelekea katika kinu cha nishati ya nyuklia, ZaporizhzhiaPicha: Dean Calma/IAEA/abaca/picture alliance / abaca

Ukraine na Urusi zimekuwa zikitupiana lawama ya kukishambulia kinu hicho kikubwa kabisa cha nishati ya nyuklia barani Ulaya, ambacho kinatarajiwa kutembelewa na timu ya waangalizi wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA inayoongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi.

Mawaziri wa Ulinzi wa Ulaya kukutana

Wakati huo huo, mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wameonekana kugawanyika kuhusu mpango wa kutoa mafunzo makubwa kwa vikosi vya Ukraine. Wiki iliyopita, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell alipendekeza kuwepo kwa kikosi cha umoja huo kitakachotoa mafunzo hayo. Mawaziri hao wanakutana kuanzia Jumanne kwa mkutano wa siku mbili mjini Praque kuuzungumzia mpango huo.

Ama kwa upande mwingine, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema hatua za serikali kuhakikisha usambazaji wa gesi wakati wa majira ya joto zimeitayarisha Ujerumani kukabiliana na vizuizi zaidi vya usambazaji wa gesi kutoka Urusi. Matamshi hayo ameyatoa Jumanne, siku moja kabla Urusi haijasitisha usambazaji wa gesi kwa siku tatu.

(AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW