1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Shambulizi la Urusi lawaua watu 7 na kujeruhi 100 Ukraine

19 Agosti 2023

Urusi imefanya shambulio kwenye mji wa Ukraine wa Chernihiv, ambao ni makao makuu ya mkoa wa kaskazini mwa nchi hiyo wenye jina sawa na hilo.

Ukraine | Chernihiv
Maafisa wa uokoaji katika eneo kulikoshambuliwa mjini ChernihivPicha: VALENTYN OGIRENKO/REUTERS

Wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema shambulio hilo, limesababisha vifo vya watu 7 na kuwajeruhi wengine 100. Mji huo ulioko kilometa takriban 150 kaskazini mwa mji mkuu wa Kiev kuelekea Belarus, kwa kiasi kikubwa haukuwa umelengwa na mashambulizi mazito kuanzia miezi ya kwanza ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

Taarifa za hujuma hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine, Ihor Klymenko. Rais Zelensky amelaani shambulio hilo, ambalo amesema liliyalenga majengo ikiwemo ukumbi wa burudani na chuo kikuu.

"Hivi ndiyo iliyo kuwa jirani na taifa la kigaidi, hili ndiyo linafanya tuiunganishe dunia nzima kulipinga. Kombora la Urusi limepiga katikati ya mji wetu wa Chernihiv" ameandika rais Zelensky kupitia ukurasa wake wa Telegram.

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine (kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Sweden, Ulf Kristersson huko Harpsund, Sweden Picha: Jonas Ekstromer/TT News Agency/REUTERS

"Uwanja wa umma, chuo cha ufundi stadi na ukumbi wa sanaa. Jumamosi tulivu ambayo Urusi imeibadili kuwa siku ya maumivu na hasara" ameongeza kiongozi huyo.

Ziara ya Zelenksy Sweden

Wakati Urusi ikifanya shambulio hilo, Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine ameitembelea Sweden siku ya Jumamosi, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu Urusi ilipoivamia nchi yake mwaka jana. Serikali ya Sweden ilisema Zelensky atakutana na maafisa wa nchi hiyo kwenye mji wa Harpsund, kiasi kilometa 120 kutoka mji mkuu Stockholm. Kadhalika ameandaliwa mkutano na Mfalme Carl XVI Gustaf na Malkia Silvia kwenye kasri moja kwenye mji huo.

Sweden iliutelekeza msimamo wake wa miongo kadhaa wa kutofungamana na upande wowote duniani kijeshi na kuamua kuisaidia Ukraine kwa kuipatia silaha na msaada mwingine wa kijeshi kuiwezesha kupambana na Urusi.

Kadhalika taifa hilo liliomba mara moja uanachama ndani ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hivi sasa inasubiri idhini ya kujiunga rasmi.

Putin akutana na makamanda wa jeshi wanaoongoza vita

Rais Vladimir Putin wa Urusi Picha: Alexander Kazakov/AP Photo/picture alliance

Nchini Urusi rais wa Urusi Vladimir Putin amewatembelea makamanda wa ngazi ya juu wanaoongoza vita kwenye mji wa Rostov-on-Don, karibu na mpaka wa Ukraine. Taarifa hizo zimetolewa na Ikulu ya Kremlin.

Mji huo ulioko kusini mwa Urusi umekuwa kitovu cha oparesheni za vikosi vya Moscow nchini Ukraine.

Hata hivyo, Kremlin haikutoa maelezo ya lini mkutano huo umefanyika lakini kulingana na video zilizoonyeshwa na vyombo vya habari vya taifa, zinaashiria kwamba mazungumzo hayo yamefanyika usiku.

Mkutano huo wa Putin na Majenarali umefanyika baada ya Marekani kuidhinisha upelekwaji wa ndege za kivita chapa F-16 za Uholanzi na Denmark nchini Ukraine.

Putin ameonekana akisalimiana na mkuu wa kikosi cha wanajeshi wa Urusi Valery Gerasimov ambaye hajaonekana sana hadharani tangu uasi wa kundi la Wagner ambalo lilikuwa linataka aondolewe.