1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Shambulizi la Urusi lawauwa watu 6 Donetsk, nchini Ukraine

28 Agosti 2024

Mashambulizi ya mabomu ya Urusi katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine yamesababisha vifo vya watu sita leo wakati ambapo Urusi imetangaza kukiteka kijiji kingine katika eneo hilo.

Shambulizi la Urusi mjini Kyiv nchini Ukraine mnamo Julai 8,2024
Shambulizi la Urusi mjini Kyiv nchini UkrainePicha: Ori Aviram/Middle East Images/AFP/Getty Images

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii hii leo asubuhi, gavana wa eneo la Donetsk Vadym Filashkin amesema vikosi vya Urusi vimewauwa watu wanne na kuharibu nyumba moja huko Izmailivka.

Filashkin ameongeza kuwa watu wawili zaidi waliuawa katika mashambulizi tofauti karibu na Chasiv Yar ambayo yaliharibu zaidi ya nyumba 12.

Vikosi vya Urusi vyateka eneo lingine la Ukraine

Wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza leo kwamba vikosi vyake vimeteka makazi mengine umbali wa kilomita 20 kutoka eneo la shughuli nyingi la Pokrovsk.

Hivi karibuni, mamlaka za kikanda zimeamuru uhamishaji mkubwa wa lazima wa watu huku vikosi vya Urusi vikisonga mbele kuelekea Pokrovsk, eneo lililokuwa makazi ya takriban watu 60,000.

Soma pia:Urusi yafanya mashambulizi makubwa dhidi ya Ukraine.

Filashkin amesema watu 2,718 wanaowajumuisha watoto 392 wamehamishwa kutoka maeneo yalioko katika mstari wa mbele wa vita.

Baadaye kupitia shirika la habari la serikali, Filashkin alisema baadhi ya watu 30,000 walisalia Pokrovsk na vijiji vya karibu na kwamba benki zitafungwa mjini humo kufikia siku ya Jumapili.

Zelensky asema mkataba na kampuni ya Urusi ya Gazprom hautarefushwa

Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema jana kwamba nchi yake haitarefusha makubaliano ya kusafirisha gesi ya Urusi kwenda Ulaya kupitia nchi hiyo baada ya Desemba 31.

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry PeskovPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Akizungumzia uamuzi huo, msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov amesema kuna njia mbadala lakini maamuzi hayo ya Ukraine yatasababisha athari kubwa kwa maslahi ya wateja wa Ulaya ambao bado wanataka kununua gesi ya Urusi.

Mataifa kadhaa ya EU bado yanapokea gesi ya Urusi kupitia Ukraine

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya ya Austria, Hungary na Slovakia bado yanapokea gesi ya Urusi kwa njia hiyo.

Nchi hizo tatu zinaendelea kutegemea gesi ya Urusi licha ya ahadi ya Umoja wa Ulaya ya kuacha utegemezi wa gesi ya Urusi ifikapo mwaka 2027 kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.

Washirika wa Ukraine wanaogopa kuidhinisha sera mpya kusaidia Ukraine 

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema leo kwamba tatizo kubwa linaloikabili Ukraine inapopambana na Urusi ni kwamba washirika wake wanaogopa kuidhinisha sera mpya kusaidia Ukraine kutokana na hofu ya kuongezeka kwa vita hivyo.

Ukraine ina nia ya kuendelea kushikilia maeneo ya Urusi kwa muda

Naibu mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA David Cohen, amesema leo kwamba vikosi vya Ukraine vina nia ya kuendelea kushikilia maeneo ya Urusi iliyoteka kwa muda fulani na kwamba shambulizi la kisasi la kushtukiza kutoka Urusi litakuwa gumu.

Akilihutubia kongamano la kijasusi, Cohen amesema Rais Putin atalazimika kukabiliana na shauku ya umma nchini mwake kwa kupoteza baadhi ya maeneo ya Urusi.