1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Urusi lawauwa watu watano nchini Ukraine

24 Machi 2026

Watu watano wameuawa leo nchini Ukraine kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya usiku kucha ya makombora na droni za Urusi. Haya ni kwa mujibu wa mamlaka ya Ukraine.

Ukraine Poltava 2026 |shambulizi la Urusi nchini Ukraine
Shambulizi la Urusi mjini Poltava Ukraine mnamo Machi 24, 2026Picha: Press service of the State Emergency Service of Ukraine in Poltava region/Handout/REUTERS

Kwenye ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa Telegram, jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha droni 392 na makombora 34 kuelekea nchini humo lakini likadungua droni 365 na makombora 25.

Ving'ora vilisikika usiku kucha karibu nchi nzima, huku mashambulizi hayo yakiua watu wawili huko Poltava, wakati Zaporizhzhia, Kherson na Kharkiv kila moja ikiripoti kifo kimoja.

Zelensky alitoa onyo kabla ya shambulizi la Urusi

Mkesha wa mashambulizi hayo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kupitia hotuba yake ya kila siku kwa njia ya video, alikuwa ameonya kwamba kuna habari za kijasusi kuwa huenda Urusi inajiandaa kwa mashambulizi makubwa.

Leo asubuhi, kituo cha habari cha Suspilne Poltava, kimechapisha picha zinazoonyesha majengo ya makazi yenye madirisha yaliolipuliwa na kuta zilizoteketea.

Kulingana na huduma za dharura, watu wawili waliuawa na wengine saba kujeruhiwa katika eneo hilo.

Mkuu wa jeshi wa eneo hilo la Poltava Ivan Fedorov, amesema upande wa kusini, Urusi ilifanya mashambulizi makubwa ya droni na makombora Zaporizhzhia na mtu mmoja ameripotiwa kuuawa huku wengine watano wakijeruhiwa.

Mkazi mmoja wa eneo hilo Elen Loban ameelezea kuhusu mashambulizi hayo ya droni na makombora:

''Nilisikia ikiruka na kisha mlipuko. Tuliruka kutoka kitandani na kukimbia bila viatu. Majirani zetu walituvuta nje kupitia madirisha. Mlango huu hapa, ulikuwa umewaka moto kabisa.''

Miili ya wakazi wawili wa Zhaporizhia waliouawa katika shambulizi la Urusi mnamo Machi 21, 2026Picha: REUTERS

Kwengineko, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa walinzi wake wa anga walidungua droni 55 za Ukraine katika maeneo mbalimbali usiku uliotangulia.

FSB ya Urusi yapokea taarifa za kijasusi kuhusu tishio la shambulizi la Ukraine

Shirika la habari la Urusi RIA, limeripoti leo kuwa Huduma ya Usalama ya Urusi FSB ilipokea taarifa za kijasusi kwamba Ukraine inapanga kuwashambulia maafisa wa serikali , wafanyakazi wa kijeshi wa wizara ya ulinzi ya Urusi pamoja na maafisa wa usalama.

Mnamo mwezi Februari, naibu mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Urusi Luteni Jenerali ​Vladimir Alexeyev, ‌alipigwa risasi mara tatu akiwa kwenye jengo moja la makazi huko Volokolamsk kaskazini mwa Moscow. Hata hivyo alinusurika shambulizi hilo.

Bandari ya Urusi ya Primorsk yaanza tena upakiaji wa mafuta baada ya shambulizi 

Katika hatua nyingine, Bandari ya Urusi ya Primorsk kwenye bahari ya Baltic, imeanza tena upakiaji wa mafuta yasiyosafishwa kufuatia ⁠⁠kusimamishwa kwa shughuli hiyo kutokana na mashambulizi ya droni. Haya ni kwa mujibu wa vyanzo viwili na shirika la ufuatiliaji wa data za meli LSEG.

Siku ya Jumapili, bandari mbili kuu za Urusi katika Bahari hiyo ya Baltic Primorsk na Ust-Luga, zilisitisha shughuli zake kufuatia mashambulizi ya droni.

Ust-Luga ilianza tena usafirishaji nje wa bidhaa jana Jumatatu.

Moldova yatangaza kukatika kwa njia kuu ya umeme

Moldova imetangaza leo kwamba njia yake kuu ya umeme na Ulaya ilikatizwa kufuatia shambulizi la usiku kucha la Urusi nchini Ukraine na imewataka raia wake kutumia nishati kwa busara wakati wa masaa ya uhitaji zaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW