1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Shambulizi Paris Ufaransa, watu watatu wauawa

24 Desemba 2022

Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Ufaransa Paris, baada ya risasi kufyatuliwa dhidi ya kituo cha jamii ya Wakurdi katikati ya mji huo.

Paris Schießerei in Innenstadt
Picha: SARAH MEYSSONNIER/REUTERS

Mwendesha mashtaka amesema huenda shambulizi hilo la Ijumaa limechochewa na ubaguzi wa rangi au chuki.

Mshukiwa mmoja aliyekamatwa baada ya tukio hilo, anajulikana na maafisa wa usalama. Hayo ni kulingana na ripoti ya vyombo vya habari nchini humo.

Kikitaja vyanzo vya polisi, kituo cha redio cha France Info kimeripoti kwamba mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 69 alifahamika kwa majaribio mawili ya awali ya mauaji.

Gazeti la Le Parisien limeandika kwamba mshukiwa huyo raia wa Ufaransa alishambulia kambi ya wahamiaji kwa upanga mwaka uliopita na aliwajeruhi watu kadhaa. Mshukiwa huyo alitoka jela katikati ya mwezi wa Disemba na bado alikuwa chini ya uangalifu wa mahakama.

Maafisa wa polisi na maafisa wa kikosi cha kuzima moto wazingira eneo la mkasa ambapo watu watatu waliuawa kufuatia shambulizi dhidi ya kituo cha jamii ya Wakurdi mjini Paris ufaransa Disemba 23, 2022.Picha: SARAH MEYSSONNIER/REUTERS

Mshukiwa huyo anadaiwa kufyatua risasi katika mojawapo ya mitaa ya Paris (Wilaya ya 10) Ijumaa. Watu watatu waliuawa kwenye shambulizi hilo na wengine walijeruhiwa.

Kulingana na meya wa wilaya hiyo, Alexandra Cordebard, jamaa huyo alifyatua risasi dhidi ya kituo cha jamii ya Wakurdi na vilevile dhidi ya mgahawa na pia alifyatua risasi kwenye saluni moja eneo hilo.

Meya wa Paris, Anne Hidalgo, amesema shambulizi hilo ni kitendo cha watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Hidalgo ameandika: "Jamii ya Wakurdi na kupitia kwao, wakaazi wote wa Paris wamelengwa kwenye mauaji hayo ya wanaharakati wa misimamo mikali ya mrengo wa kulia."

"Wakurdi, popote pale wanapoishi, wanapaswa kuishi kwa amani na usalama. Zaidi ya wakati wowote ule, Paris inasimama nao katika nyakati hizi za giza,” Hidalgo ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Vurugu zilizuka baina ya waandamanaji na polisi baada ya shambulizi dhidi ya kituo cha jamii wa Wakurdi mjini Paris Disemba 23, 2022.Picha: Lewis Joly/AP Photo/picture alliance

Waziri wa ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin alisema siku ya Ijumaa kwamba Ufaransa sasa inataka kulinda maeneo ya mikutano wa Wakurdi na kwamba walinzi wanapaswa kupelekwa katika kumbi hizo kote nchini. Ameongeza kuwa balozi za Uturuki nchini humo pia zinapaswa kulindwa ili kuzuia mashambulizi ya kisasi.

Vurugu zilizuka saa chache baada ya shambulizi hilo, huku maafisa wa polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya Wakurdi waliokuwa wakiandamana wakiishutumu serikali ya Uturuki.

Ofisi ya mwendesha mashtaka imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya makusudi. Hata hivyo hakukuwa na taarifa za awali kuhusu kilichomchochea mshambuliaji.

Laure Beccuau ambaye ni mwendesha mashtaka amesema uchunguzi utatathmini ikiwa nia na misimamo ya ubaguzi wa rangi zilichochea.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shambulizi la 23.12.2022 dhidi ya kituo cha jamii ya Wakurdi mjini Paris.Picha: Lewis Joly/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema hilo lilikuwa shambulizi la makusudi dhidi ya Wakurdi.

"Wakurdi walioko Ufaransa wamelengwa kwenye shambulizi la chuki katikati ya Paris,” aliandika Macron na kuongeza kuwa mawazo yake yalikuwa na walioathiriwa pamoja na familia zao.

Kesi ya mashambulizi ya Paris 2015 yaanza

Kufuatia shambulizi hilo, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameelezea kusikitishwa kwake. "Kitendo cha kutisha kimetikisa Paris na Ufaransa leo. Mawazo yangu yako na waathiriwa na familia zao,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter usiku wa kuamkia Jumamosi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, pia aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba "Daima chuki isishinde,” akilirejelea tukio hilo.

Vyanzo: DPAE, APE