Sharaa anusurika kuuawa mara tano - Guterres
12 Februari 2026
Ripoti iliyotolewa siku ya Jumatano (Februari 11) na Guterres ilisema Sharaa alishambuliwa akiwa kaskazini mwa mji wa Aleppo na pia kusini mwa mji wa Daraa na kundi lijiitaalo Saraya Ansaru Sunnah, ambalo linafahamika kuwa sehemu ya kundi la IS.
Hata hivyo, ripoti hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi haitaji tarehe wala undani wa majaribio haya ya kumuua al-Sharaa au Waziri wa Mambo ya Ndani, Anas Hassan Khattab, na Waziri wa Mambo ya Nje, Asaad al-Shibani.
"Majaribio haya ya mauaji ni ushahidi zaidi kwamba kundi hili la wanamgambo lina dhamira ya kuihujumu serikali mpya ya Syria kwa kutumia ombwe la usalama na hali ya ukosefu wa uhakika iliyopo," ilisema ripoti hiyo.
Kwenye majaribio hayo, al-Sharaa, ambaye ameiongoza Syria tangu vikosi vyake vya waasi vilipompinduwa mtawala wa muda mrefu, Bashar al-Assad, Disemba 2024, alikuwa ndiye mlengwa mkuu.
Mwenyewe Sharaa aliwahi kuongoza kundi la Hayar Tahrir al-Sham, ambalo lilikuwa na uhusiano na kundi la al-Qaida, ingawa baadaye alisema amevunja mahusiano nalo.
Marekani yaondosha wanajeshi Syria
Marekani nayo iliripotiwa kuwaondosha wanajeshi wake kutoka kituo mji wa Al-Tanf kaskazini mashariki mwa Syria na kuwahamishia nchini Jordan.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya kile kiitwacho "muungano wa kimataifa dhidi ya kundi la kigaidi la IS" unaoongozwa na Marekani.
Chanzo kimoja kutoka jeshi la Syria kililiambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya Marekani viliondoka kwenye kituo cha Al-Tanf siku ya Jumatano.
"Wanajeshi wa Syria ndio wanaopelekwa kutwaa udhibiti wa eneo hilo," kiliongeza chanzo hicho.
Chanzo kingine kilisema kwa wiki mbili sasa, wanajeshi wa Marekani walikuwa wakiondosha vifaa vyao kidogo kidogo.
Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la IS, wanajeshi wa Marekani walipelekwa kwenye eneo linalodhibitiwa na vikosi vya Kikurdi kaskazini mashariki na Al-Tanf, karibu na mpaka na Jordan na Iraq.
Kundi la wapiganaji wa Kikurdi (SDF) lilikuwa mshirika mkubwa wa muungano huo wa kupambana na IS unaoongozwa na Marekani, lakini tangu kuangushwa kwa utawala wa Assad, Marekani imekuwa ikijikurubisha zaidi kwa utawala mpya wa Syria.
Baada ya mapigano ya mara kadhaa kati ya vikosi vya serikali ya Syria na SDF, hatimaye makubaliano yalifikiwa mwezi uliopita kwa wapiganaji wa Kikurdi kujiondosha eneo hilo na kuanza mchakato wa kuwa sehemu ya jeshi la nchi.