1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sharm El – Sheikh, Misr Polisi wapambana na watu wenye silaha.

26 Julai 2005

Polisi wa Misr wamepambana na watu wenye silaha katika milima ya jangwani karibu na mji wa kitalii ulioko katika pwani ya bahari ya Sham wa Sharm el – Sheikh jana katika juhudi za kuwatafuta watu waliohusika katika shambulio ambalo limesababisha watu 88 kuuwawa.

Siku mbili baada ya shambulio baya kabisa dhidi ya Misr tangu mwaka 1981, polisi walikuwa wamekizingira kikundi cha watu wa kabila la Bedouin ambao wanatuhumiwa kuwa wanamahusiano na watu waliolipua mabomu matatu ambayo yaliharibu hoteli na eneo la maduka katika mji huo wa kitalii.

Duru za kipolisi zimesema kuwa watu 25 kutoka kabila hilo la Bedouin wamekamatwa baada ya kurushiana risasi na polisi katika milima karibu na kijiji cha el- Ruwaisat, kaskazini mwa Sharm el – Sheikh.

Viongozi wamesema kuwa polisi wameweza kufuatilia yalikotoka magari mawili ambayo yalitumika katika mashambulio hayo ambayo yametoka katika kijiji cha kaskazini cha Ras Sidr, upande wa pwani ya magharibi ya rasi ya Sinai, wakijifanya kuwa ni wachimba mawe.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW