1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHARM EL SHEIKH: Rais Mubarak akutana na rais Abbas

25 Juni 2007

Mkutano wa pande nne kati ya kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert rais Hosni Mubarak wa Misri na mfalme Abdullah wa Jordan unatarajiwa kuanza katika mji wa pwani wa Sharm el Sheikh nchini Misri.

Mkutano huo unaazimia kutafuta njia za kuanzisha uhusiano mpya kati ya Palestina na Israel baada ya chama cha Fatah kinacho ongozwa na rais Mahmoud Abbas kujitenga na chama cha Hamas tangu chama hicho kilipoudhibiti Ukanda wa Gaza.

Muda mchache uliopita rais Hosni Mubarak amefanya mazungumzo ya pande mbili na kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Juu ya jitihada za kutafuta amani kati ya Israel na Palestina waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema.

O ton…hatufanyi hayo kwa sababu tunapendelea upande wowote tunafanya haya kwa sababu ni lazima tuwe na mshirika katika upande wa pili iwapo tunataka kuendelea na mustakabali wetu.

Hapo jana serikali ya Israel iliamua kuachilia mamilioni ya dola kwa utawala wa rais Mahmoud Abbas lakini maafisa wameeleza kuwa Israel bado inasita kuondosha vizuizi na vikwazo vinginevyo katika Ukingo wa Magharibi hadi pale utawala wa rais Mahmoud Abbas

utakapo wajibika zaidi katika kupambana na wapiganaji wenye msimamo mkali.

Wakati viongozi hao wa mashariki ya kati wakiwa wanakutana nchini Misri tawi la kijeshi la chama cha Hamas limetoa ukanda wenye sauti ya askari wa Israel Gilad Shalit alietekwa nyara siku kama ya leo mwaka jana.

Katika ukanda huo mwanajeshi huyo anaisihi Israel ikubali matakwa ya wateka nyara pamoja na kueleza kuwa afya yake inasambaratika na kwamba anahitaji matibabu.

Shalit ameilaumu serikali yake kwa kutochukua hatua thabiti ili aachiliwe huru.

Askari huyo alitekwa nyara kwenye Ukanda wa Gaza alikokuwa analinda mpaka.